RAIS SAMIA AFUNGUA MKUTANO WA MAWAZIRI WA SHERIA WA JUMUIYA YA MADOLA
Viongozi
mbalimbali waliohudhuria hafla ya kufungua Mkutano wa Mawaziri wa Sheria kutoka
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola, 04 Machi, 2024, Zanzibar.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na William Mabusi – WKS
Zanzibar
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefungua
Mkutano wa siku tano wa Mawaziri wa Sheria kutoka nchi wanachama wa Jumuiya
hiyo huku akisisitiza matumizi ya teknolojia ya kidijitali kuharakisha
upatikanaji haki.
Ufunguzi
wa mkutano huo wenye nchi wanachama hamsini na sita umefanyika leo tarehe 04
Machi, 2024 katika Hotel ya Golden Tulip Visiwani Zanzibar na kuhudhuriwa na
viongozi mbalimbali wa Serikali.
“Nashukuru
Jumuiya ya Madola kwa kuchagua nchi yetu Tanzania na hasa hapa Zanzibar
kufanyia mkutano huu mkubwa ambao unalenga kujadili pamoja na mambo mengine jinsi
maendeleo ya kidijitali yanavyowezesha uboreshaji wa upatikanaji wa haki kwa watu.” Alisema.
Mhe.
Rais amesema teknolojia za kidijitali zikiundwa na mifumo iliyorahisishwa zinamsaada
mkubwa katika kutoa njia bunifu na rahisi kwa watu kuweza kupata suluhu kupitia
mifumo rasmi na isiyo rasmi ya utoaji haki.
Akielezea
mikakati mbalimbali inayofanywa na Serikali katika kusimamia utoaji haki
amesema “Serikali ilizindua kampeni kubwa inayoitwa Mama Samia Legal Aid
Campaign kushughulikia utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria, upatikanaji wa
haki kwa wananchi katika ngazi zote, kushughulikia masuala mtambuka yanayohusu
haki za binadamu na watu, mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, ukatili
dhidi ya wanawake na watoto, masuala ya usimamizi wa ardhi, mirathi na utatuzi
wa migogoro."
Awali
akitoa hotuba ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Waziri wa Katiba na Sheria wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema chini ya
utawala wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa
katika masuala ya uzingatiaji amani, demokrasia na maendeleo.
Naye
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola MH. Patricia Scotland KC Akitoa salaam katika
mkutano huo ametoa pole kwa Tanzania kwa kuondokewa na Rais wa Awamu ya Pili
Mhe. Ali Hassan Mwinyi. “Katika mkutano huu tunaungana na Jamhuri ya Muungano
wa Tanzani katika kipindi hiki cha maombolezo ya Kitaifa kufuatia kifo cha Rais wa Awamu ya Pili, tupo
hapa Zanzibar ambapo Marehemu Rais alikuwa mwanafunzi, mwalimu na kiongozi.
Tunasikitika zaidi kwani Rais Mwinyi alikuwa ni kiongozi wa Serikali aliyeleta
mageuzi katika teknolojia kwa kuruhusu matumizi ya simu za mkononi na kompyuta na
leo tunakusanyika chini ya kaulimbiu ya teknolojia na uvumbuzi inavyoweza
kutumika ili kuwezesha upatikanaji wa haki kwa wakati kwa raia."
Mkutano huo wa Mawaziri wa
Sheria kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola unafanyika nchini kwa mara ya
kwanza, utahitimishwa tarehe 8 Machi, 2024 ambapo Mgeni Rasmi siku hiyo anatarajiwa
kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein
Ali Mwinyi.
Comments
Post a Comment