SUALA LA MIRADI YA SERIKALI KUTOZWA KODI KUFIKISHWA BUNGENI
Waziri wa
Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akiongea kabla ya kumkaribisha
Mwenyekiti wa Kamati wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala,
Katiba na Sheria Mkoani Iringa, 12/03/2024.
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel akiwasilisha taarifaa ya
utekelezaji wa Mahakama wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Utawala, Katiba na Sheria mkoani Iringa leo 12/03/2024.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria pamoja na Watendaji wa Mahakama na viongozi wa Wizara wakiwa katika picha ya pamoja baada ya ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria mkoani Iringa leo 12/03/2024.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na Lusajo Mwakabuku – WKS IRINGA
Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Joseph
Mhagama amesema ni wakati sasa Serikali kuangalia kama kuna tija katika kutoza
miradi ambayo inatengenezwa kwa ajili ya wananchi kwani kufanya hivyo si kwamba
kunaongeza mlolongo wa utekelezaji wa miradi hiyo peke yake bali pia kunaongeza
gharama katika kupitia hatua za upatikanaji wa msamaha wa kodi katika miradi ya
Serikali.
Mhe. Mhagama
ameyaongea hayo baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa
Mahakama katika Mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma tarehe 12 Machi, 2024 ikiwa
ni sehemu ya ziara ya Kamati hiyo katika kukagua miradi ya maendeleo kwa
taasisi zilizo chini ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria.
Mhe. Mhagama
alisema kuwa kwake anaona suala hilo halina tija na ni ajenda watakayoenda nayo
bungeni kwani tayari hiyo miradi inaandaliwa kwa lengo la kumsaidia mwananchi
hivyo hata makusanyo ya kodi hizo ni kwamba mapato yake yanarudi katika kumhudumia
mwananchi hivyo ni bora badala ya fedha hizo kurudi hazina zitumike katika
kuharakisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
“Kwanza
ngoja niwaambie kupatikana kwa msamaha wa kodi ni process, ina mlolongo
wake mrefu ambao umesababisha baadhi ya miradi kutoendelea kwa zaidi ya mwaka
kusubiria mchakato huo kukamilika. Hela zenyewe zote ni za Serikali ni sawa
na kutoa fedha mkono wa kulia kuhamishia
mkono wa kushoto. Mbaya zaidi tunachelewasha huduma kwa wananchi wakati wa
kufuatilia msamaha hii ya kodi.” Alisema Mhe. Mhagama.
Awali
akimkaribisha Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Joseph Mhagama na kamati yake,
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana alisema anamshukuru
Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha miradi mbalimbali ndani ya Wizara ya Katiba
na Sheria inayolenga kusogeza karibu miundombinu ya utoaji haki kwa wananchi
ikiwemo miradi ya ujenzi wa mahakama mbalimbali nchini huku akibainisha kwamba
suala hili limeendelea kuongeza imani kwa wananchi kuhusu mahakama ikiwemo
matumizi ya teknolojia katika usajili na uendeshaji kesi unaorahisisha kesi
nyingi kusikilizwa ndani ya muda mfupi.
Mhe. Chana
alisema “kama moja ya jitihada za kupunguza kero kwenye baadhi ya maeneo yenye
watu na migogoro mingi mahakama ilikuja na wazo la Mahakama inyotembea yaani
Mobile Court. Kwa jitahada hizo, tumefanikiwa kupunguza mrundikano wa Mashauri
hadi kufikia 4%.”
Waziri Chana
pia akaongeza “Tume ya Kuboresha Haki Jinai imependekeza namna tunavyoweza
kuboresha upatikanaji haki kwa masuala ya Jinai ambayo Wizara yetu imeyachukua
na inayafanyia kazi ikiwemo matumizi ya TEHAMA kwa upande wa Mahakama kwa mfano
mfumo wa mashauri ufahamikao kama Advance Case Management System ambao
umeunganishwa na mifumo kadhaa ya wadau, mfumo wa kutafsiri na kutunza
kumbukumbu na pia kusikiliza mashauri kwa njia ya Video yaani Video Conference Board.”
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel akiwasilisha taarifa ya utekelezaji
wa Mahakama alisema “kufanikiwa kwa Mahakama kunatokana na uongozi mzuri wa
Jaji Mkuu ambaye ana maono makubwa, lakini pia ushrikiano mkubwa wa mihimili
mitatu ndio unaopelekea utekelezaji wa majukumu yetu kuwa rahisi katika kutoa
huduma.”
“Hadi hivi
sasa tumefanikiwa kujenga Mahakama za mwanzo 960 na lengo likiwa ni kufikia Mahakama
3000 nchini kote. Hivi sasa tuna wilaya 139 lakini mahakama zipo 135
zimebakia mahakama 4 tu katika kuhakikisha kila wilaya ina Mahakama
nchini. Aidha, katika Ukanda wa Kusini
na Mashariki mwa Afrika, Mahakama ya Tanzania ndio inaongoza katika matumizi ya
TEHAMA katika utoaji haki kwa wananchi. Hivi sasa Hakimu anaweza maliza kesi
halafu akapata nakala ya kesi ya kurasa 200 chini ya dakika mbili kwa Kiswahili
kupitia mfumo wa AI” Alisema Ole Gabriel.
Katika utekelezaji wa miradi hiyo, Mtendaji Mkuu wa
Mahakama aliongeza kuwa katika viwango vya ubora wa usimamizi wa miradi ya Mahakama
vilivyowekwa na Benki ya Dunia katika miradi yake, Tanzania imefikia asilimia
89 ya ubora wa utekelezaji wa miradi, kiwango ambacho ni cha juu zaidi duniani
katika miradi ya Mahakama inayotekelezwa na Benki ya Dunia.
Akielezea changamoto za Wakandarasi katika miradi hiyo,
Mtendaji Mkuu wa Mahakama alisema kuna baadhi ya Wakandarasi ambao walipewa
kazi nao wakawapa kazi watu wengine na mbaya zaidi wakawa hawana taarifa yeyote
juu ya uendelezwaji wa miradi husika suala lililopelekea Mtendaji wa Mahakama
kugoma kulipa mpaka suala hilo liwekwe sawa.
Akihitimisha ziara hiyo mkoani Iringa, Mhe. Mhagama
alisifia utendaji wa Mahakama na kwamba wao kama kamati ya taasisi hizi
wanatembea kifua mbele kutokana na ubunifu,
na utekelezaji wa miradi aidha akaiagiza Mahakama kuangalia namna ya
kugawanya masurufu katika utekelezaji miradi kwa kuanzia na Tarafa, Majimbo na
hatimaye Kata katika kujenga Mahakama.
“Tutashirikiana na Wizara kuhakikisha kuwa bajeti ya Mahakama
inakidhi mahitaji kwani ndio muhimili pekee wenye kazi kubwa katika kuhakikisha
utulivu na amani inapatikana nchini”. Alisema Mhe. Mhagama.
Comments
Post a Comment