MASHAURI 705 YAOKOA TRILIONI 3.4 FEDHA ZA SERIKALI

 

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano wa pili wa Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Aprili 19, 2024 Mkoani Morogoro.


Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi  akisoma hotuba wakati wa ufunguzi wa mkutano wa pili wa Baraza la pili la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Aprili 19, 2024 Mkoani Morogoro.

Kaimu Naibu Wakili  Mkuu wa Serikali Ndg. Mark  Mulwambo akizungumza wakati wa ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi, Aprili 19, 2024 Mkoani Morogoro.

Naibu Waziri wa  Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini (katikati) akiongoza zoezi la kuimba wimbo wa mshikamano ikiwa ni ishara rasmi ya kuanza kwa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali. Pamoja naye ni Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende (wa kwanza kulia kwake), Kaimu Naibu Wakili Mkuu wa Serikali  Ndg. Mark  Mulwambo (wa pili kulia)  pamoja na viongozi wengine wa Baraza hilo. Aprili 19, 2024 Mkoani Morogoro.

Baadhi ya Watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakifuatilia hotuba ya Mgeni Rasmi ambaye ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini katika ufunguzi  wa mkutano wa pili wa Baraza la pili la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Aprili 19, 2024 Mkoani Morogoro.


Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini (kushoto) akipokea zawadi  kutoka kwa Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende (kulia) mara baada ya kukamilika kwa kufungua mkutano wa pili wa Baraza la pili la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Aprili 19, 2024 Mkoani Morogoro.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali mara baada ya kufungua  mkutano wa pili wa Baraza la pili la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Aprili 19, 2024 Mkoani Morogoro.

xxxxxxxxxxxxxxxxx

Na Yasinta Kisima – WKS Morogoro

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini ameipongeza Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika kusimamia na kushinda  Mashauri 705 yenye madai ya fedha na kuipelekea Serikali kuokoa zaidi ya Shilingi Trilioni 3.47 kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Aprili 2024.

Mhe. Sagini ameyasema hayo Aprili 19, 2024 wakati akifungua  kikao cha pili cha Baraza pili la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 katika ukumbi wa mikutano wa NSSF, Mkoani Morogoro.

"Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imeonesha uzalendo na weledi katika kuhahikisha Serikali inashinda katika Mashauri na usuluhishi ndani na nje ya nchi. Fedha ambazo zimeokelewa ni mchango mkubwa katika kuisaidia Serikali kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo. Niwapongeze kwa hatua hii na niwasihi tuendelee kulipigania Taifa." Alisema Mhe. Sagini.

Aliendele kusema "Tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi inavyoiwezesha Ofisi hii. Ongezeko la bajeti kutoka Shilingi Bilioni 17 zilizotengwa mwaka 2023/2024 hadi kufikia ukomo wa Shilingi Bilioni 20.7 kwa mwaka 2024/2025 ongezeko la takribani shilingi Bilioni 3.6 ni ishara kubwa kwamba Mhe. Rais anatambua mchango mkubwa wa Ofisi hii katika kuiwakilisha Serikali na Taasisi zake katika mashauri ya madai na usuluhishi"

Katika hatua nyingine Mhe. Sagini amesema kupitia mikakati ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika kushughulikia mashauri ya ardhi Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kushirikiana na Wizara ya Ardhi ili kuendelea na jitihada za kupunguza migogoro ya ardhi  kwa kuyashughulikia mapema kabla ya kuwasilishwa Mahakamani au katika mabaraza ya ardhi.

Kwa upande wake Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende  amesema kuwa Ofisi imeendelea kuwajengea uwezo Watumishi kwa kuwapatia mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi ikiwemo mafunzo ya kiubobevu katika maeneo maalumu ambapo kwa kipindi cha Julai 2023, hadi Aprili 2024 jumla ya Watumishi 11 wamepatiwa ufadhili wa mafunzo ya muda mrefu na watumishi 56 walipatiwa mafunzo ya muda mfupi ndani na nje ya nchi.

Aidha, Dkt. Luhende amesema upo uhitaji mkubwa wa Mawakili wenye ubobevu katika maeneo ya gesi, mafuta, uwekezaji, anga, madini, uchumi wa bluu, TEHAMA ili kuiwezesha Ofisi hiyo kufanya vizuri zaidi katika maeneo hayo ya kimkakati.

 Awali akiwasilisha agenda kuu ya kikao hicho, Kaimu Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Ndg. Mark. Mulwambo amesema kuwa kikao hicho kinalenga kupitia na kujadili makadirio ya mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ambapo makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka huo ni Shilingi 20,750,720,000. Ofisi ikitaraji kutumia Shilingi Bilioni 4.3 na matumizi mengineyo yakitarajiwa kuwa Shilingi Bilioni 16.4.

Ikumbukwe kuwa, Mabaraza ya Wafanyakazi mahala pa kazi ni nyenzo muhimu katika kuboresha utendaji na ufanisi wa utekelezaji wa majukumu kwa Wafanyakazi.




Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA