SAGINI AFURAHISHWA NA MAPOKEZI MoCLA
Naibu Waziri mpya wa Katiba na
Sheria Mhe. Jumanne Sagini akihutubia Watumishi wa Wizara hiyo alipopokelewa
kwa mara ya kwanza Wizarani hapo, tarehe 08 Aprili, 2024 Ofisi za Wizara Mtumba
Dodoma.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini akisalimiana na Watumishi wa Wizara baada ya kupokelewa Wizarani hapo, tarehe 08 Aprili, 2024.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akimkabidhi Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini ua alipopokelewa Wizarani hapo, tarehe 08 Aprili, 2024.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana pamoja na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini wakati wa iftar, tarehe 08 Aprili, 2024.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Wizara ya katiba na Sheria Bw. Michael Masanja wakati wa Iftar, tarehe 08 Aprili, 2024.
Na William Mabusi – WKS Dodoma
Naibu Waziri mpya wa Katiba na
Sheria Mhe. Jumanne Sagini amestushwa na mapokezi makubwa yaliyofanywa na
Viongozi wa Wizara hiyo pamoja na Watumishi na kukiri kuwa hiyo ni mara yake ya
kwanza kukutana na mapokezi makubwa kiasi hicho.
Mhe. Sagini ameyasema hayo
wakati akiongea na Watumishi wa Wizara hiyo alipopokelewa kwa mara ya kwanza
Wizarani hapo tarehe 8 Aprili, 2024 baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo.
“Haya ni mapokezi ambayo
nilikowahi kupita sijawahi kukutana nayo, lakini Wizara ya Katiba na Sheria mko
vizuri sana, napokea mapokezo hayo kama ishara ya mahusiano mema, ambacho ni
kitu kizuri kwenye utumishi wa umma katika kufikia malengo ya taasisi.”
Mhe. Sagini amesisitiza upendo
mahala pa kazi huku akionya kwamba kufanya kazi kwa upendo haina maana kumezea
yale mabaya “tukifanya kazi kwa upendo matokeo yatakuwa mazuri sana, upendo kwa
wenzetu haina maana kumezea ya hovyo, kuchukua hatua dhidi ya maovu pia ni
upendo. Ili kuleta mwenendo mzuri unaotakiwa, wanao tenda mema lazima waone
waliofanya vibaya wanakemewa, wanaelekezwa kubadilika au wanachukuliwa hatua
stahiki kulingana na matendo yao vinginevyo hakuna maana ya anayetenda mema
aendelee kutenda mema.”
Katika kuielewa Wizara hiyo
inavyofanya kazi amesema “nitajifunza kwa kasi kazi za Wizara ili kutimiza
matarajio ya Waziri Pinda, matarajio ya watumishi lakini pia kutimiza matarajio
ya Mhe. Rais na Watanzania kwa ujumla.” Aidha, amewataka Watumishi na Viongozi
wenzake kumpa ushirikiano ili dhamira ya Rais ya kumpeleka Wizarani hapo iweze
kuzaa matunda.
Awali akimkaribisha Naibu
Waziri, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema yeye na
timu nzima ya watumishi wa Wizara wanamtakia majukumu mema na kwamba wako tayari
kufanya kazi naye ili kutoa matokeo nyanya kwenda na kasi ya Mhe. Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan.
Baada ya mapokezi hayo
watumishi na Viongozi wa Wizara walijumuika kwenye iftar iliyoandaliwa na
Waziri wa Katiba na Seria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana na Katibu wa Wizara hiyo
Bi. Mary Makondo, ikiwa ni Sadaka ya kuwafuturisha Watumishi, Wana Dododma na
wageni mbalimbali walioalikwa.
Iftar hiyo iliambatana na dua
ya kumwombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan, Mawaziri na Viongozi Waandamizi wa Serikali.
Akiongea katika iftar hiyo, Sheikh
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mustafa Rajabu Shabani amesema “Kipindi hiki Viongozi
wameutendea haki Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuanzia kwa mhe. Rais mwenyewe, Mawaziri
na Viongozi mbalimbali wa Serikali ndiyo maana nchi yetu ina amani na utulivu
ikiwa na majibu ya Mungu kwa matendo mema ya Viongozi wanayofanya katika nchi
yetu.”
Comments
Post a Comment