UJENZI WA MAHAKAMA ZA WILAYA NA ZA MWANZO UNAENDELEA – SAGINI
Na William Mabusi – WKS Dodoma
Naibu
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini amesema Serikali inaendelea
kutekeleza Mpango wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama kwa awamu kote
nchini.
Mhe.
Sagini ameyasema hayo wakati akijibu swali kutoka kwa Mbunge wa Kalambo Mhe.
Josephat Sinkamba Kandege Bungeni tarehe 16 Aprili, 2024 Jijini Dodoma.
Katika
swali lake la msingi lililoulizwa na Mhe. Rashid Shangazi kwa niaba yake, Mhe.
Kandege alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kujenga na kukarabati
Mahakama za Mwanzo Wilayani Kalambo.
Katika
kuweka msukumo wa ujenzi wa majengo ya Mahakama kote nchini Mhe. Sagini amesema
”Serikali ina Mpango wa ukarabati na ujenzi wa Mahakama kwa awamu. Kupitia
Mpango huo katika mwaka wa fedha 2019/20 imeshajengwa Mahakama ya Mwanzo ya Msanzi
katika jimbo la Kalambo. Pia katika mwaka wa fedha 2023/24 Mahakama ya Wilaya pamoja
na Mahakama ya Mwanzo ya Kasanga zinajengwa.”
Akijibu swali la nyongeza
lililoulizwa na Mhe. Shangazi aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani mahususi
wa kukarabati Mahakama ya Mwanzo au kujenga Mahakama mpya kwenye Tarafa ya
Mlalo, Mhe. Sagini amesema katika Mwaka wa fedha 2024/25 jumla ya Mahakama za Mwanzo
72 ziko kwenye mpango wa kukarabatiwa hivyo atawasiliana na Mtendaji Mkuu wa Mahakama
kujua Mahakama hiyo imewekwa awamu ipi.
Comments
Post a Comment