ACHANENI NA MISIMAMO HASI – DC MAKETE
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto,
Polisi Wilaya ya Makete Afande Nicholous Chilemile akitoa mada ya ukatili wa kijinsia
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Ihela Kata ya Tandala katika
kutekeleza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, Mei 28, 2024.
Afisa Maendeleo Halmashauri ya
Wilaya ya Makete Bw. Henry Nyigu akitoa mada ya haki na wajibu wa mtoto kwa
wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Ihela, Mei 28, 2024 Kata ya Tandala.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na William Mabusi – WKS Makete
Mkuu wa Wilaya ya Makete Bw. Juma
Sweda amewaasa wananchi kuacha misimamo hasi na kukubali ushauri wanaopewa na
Wataalamu wanaotekeleza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwani
misimamo mingine inaenda kinyume na sheria na hivyo kuendelea kuchangia
migogoro katika jamii.
Mkuu huyo wa Wilaya ameyasema
hayo Mei 28, 2024 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Ihela na
baadaye kwenye Kijiji cha Ikonda wakati alipotembelea timu inayotekeleza
Kampeni hiyo katika Halmashauri ya Wiliaya ya Makete na leo kampeni hiyo
ilikuwa inatekelezwa kwenye Kata ya Tandala.
“Unaweza kuwa na msimamo wako
lakini kumbe msimamo huo ni kinyume na Sheria kitu ambacho kitapelekea uendelee
kuishi kwenye mgogoro usioisha halafu kuendeleza uhasama na visasi kwenye jamii. Hivyo nawasihi wananchi mkubali
kushauriwa na kubali kuachia misimamo isiyo na manufaa kwani kwa kufanya hivyo utaruhusu
furaha na amani kuingia moyoni kwako.” Alisema.
Mkuu huyo wa Wilaya aliendelea
kuwasihi wananchi kueleza bila woga wala wasiwasi changamoto zozote za
kifamilia, ardhi na shida zingine za kisheria ili wasaidiwe na wataalamu hao.
Aidha, alisema wataalamu watawashauri viongozi wao pale tu watakapokuwa
wameelewa vizuri changamoto za wananchi.
Akitoa mada ya ukatili wa
kijinsia, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto, Polisi Wilaya ya Makete Afande
Nicholous Chilemile amesema ”kweli sisi wanadamu si Malaika hivyo makosa yapo,
lakini Serikali inatoa kampeni kama hizi kutoa elimu ili watu wawe na uelewa wa
sheria. Tunapobaini kufanyika kwa matendo haya tutoe taarifa kwenye vyombo vya
sheria ili wahusika wachukuliwe hatua,” alisema huku akiwaomba wananchi
kuchukua hatua mapema kitu ambacho husaidia katika uchunguzi badala ya kuanza
kuyamaliza kifamilia baadaye wakishindwa kuelewana ndo wanaenda kwenye vyombo
vya sheria kitu ambacho hupelekea kupotea kwa ushahidi.
Akijibu swali la Bw. Daniel
Kisimbila Sanga wa kijiji cha Tandala aliyetaka akina baba nao wawe na dawati
lao kwani nao wanachangamoto na hawajui pa kuzipeleka amesema Dawati la Jinsia
ni kwa watu jinsia zote.
Aidha, Afande Nicholous amewaasa
wazazi kujenga urafiki na watoto wao ili iwe rahisi mtoto kujieleza kwa wazazi
pale anapokabiliana na vitendo vya ukatili jambo ambalo litasaidia katika
kuwalinda watoto.
Comments
Post a Comment