MSLAC IMESAIDIA KUSUKUMA MASHAURI MENGI YA JINAI – DPP MWAKITALU
Hyasinta Kissima-WKS Njombe
Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini
(DPP) Sylvester Mwakitalu, amesema kuwa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama
Samia imesaidia kusukuma mashauri mengi ya jinai kutokana na malalamiko na
mapendekezo ambayo wamekuwa wakiyapokea kutoka kwa wadau wao.
Mwakitalu aliyasema hayo mjini
Njombe mara baada ya kutembelea katika Gereza la Njombe na kuzungumza na
mahabusu na wafungwa waliopo katika Gereza hilo.
"Katika mikoa ambayo
kampeni hii imeshafanyika na sasa katika mkoa wa Njombe, tumekwenda kwenye Magereza,
tumekwenda kwenye mahabusu za watoto kuna mambo mengi yameibuka na mengi
tumeyafanyia kazi. Zipo baadhi ya kesi zimesimama haziendelei, kutokana na
sababu mbalimbali lakini baada ya kusikia na kupokea malalamiko na maelekezo
kutoka kwa wadau mengi tumeyapatia ufumbuzi."Alisema Mwakitalu
DPP Mwakitalu amesema kuwa
Kampeni ya Msaada wa Kisheria imesaidia sana kusukuma mashauri mengi ya Jinai
kwa wateja wanaowahudumia ikiwa ni pamoja na watuhumiwa, waathirika wa
makosa hayo na mashahidi.
Rai imetolewa kwa Wananchi
kufika katika Ofisi za Mkurugenzi wa Mashtaka zilizopo katika makao makuu ya
Mikoa yote Tanzania Bara na Ofisi katika wilaya 62 kwa ajili ya kupata ushauri
na kuwasilisha malalamiko yao katika mashauri mbalimbali ili kupata ushauri wa kitaalamu.
Comments
Post a Comment