MSLAC ITUMIKE KUTAFUTA SULUHU NA SIO MSHINDI
Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko akihutubia wakati wa uzinduzi
wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Mkoani Njombe, Mei 26, 2024.
Katibu
Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo akitoa salaam wakati wa uzinduzi
wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Mkoani Njombe, Mei 26, 2024.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na Hyasinta Kissima – WKS Njombe
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko amewataka watoa huduma za Msaada wa Kisheria
kuitumia kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika kufanya
utatuzi wa migogoro badala ya kutafuta mshindi miongoni mwa jamii.
Dkt. Biteko aliyasema hayo Mei
26, 2024 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia
(Mama Samia Legal Aid Campaign) Mkoani Njombe iliyofanyika katika
Halmashauri ya Mji ya Njombe.
Dkt. Biteko amesema kuwa, ni
vyema Wananchi kuacha misimamo iliyopitiliza wakati timu ya Mawakili
itakapokuwa inawasikiliza na badala yake wasimamie kwenye ukweli.
“Maandiko yanasema ukijua
kweli itakuweka huru nawe utakuwa huru kweli kweli na mawakili simamieni ukweli
mtapokuwa mnasikiliza watu hawa watakaokuja kwenu,” alisema Dkt. Biteko.
Aliendelea kusema, “Migogoro
iliyopo ya jamii miongoni mwenu iweze kuisha bila ya kusababisha madhara
makubwa, ukiona mahali fulani mtu amenyanyua upanga akamuumiza mtu mwingine,
ukiona mahali fulani mtu ameamua kumuua mtu mwingine ujue kuna shida. Ukiona
mahali fulani mtu ameamua kumfanyia ukatili mtu mwingine au mahali fulani mtu
ameamua kumnyanyasa mtu mwingine ni kwa sababu kuna mazingira ya kutokutambua
wajibu wa kila mmoja miongozi mwa jamii.” Alisema Dkt. Biteko.
Alisema Rais Samia Suluhu
Hassan aliunda Kamati ya Tume ya Haki Jinai ambayo lengo lake lilikuwa ni
kuboresha mfumo wa upatikanaji wa haki kwa umma.
“Tume ile ilikuja na
mapendekezo iliona mambo mengi ndani ya jamii na migogoro mingi ambayo ipo
kwenye jamii, miongoni mwa migogoro hiyo ni migogoro ya ardhi, masuala ya
mirathi, na utawala bora maana yake sisi viongozi tumekuwa sehemu ya migogoro
hiyo,” alisema Dk. Biteko.
Waziri wa Katiba na Sheria
Dkt. Pindi Chana alisema tangu kuzinduliwa kwa kampeni ya msaada wa Kisheria ya
Mama Samia jumla ya mikoa saba imefikiwa.
Dkt. Chana aliitaja mikoa hiyo
kuwa ni Ruvuma, Shinyanga, Singida, Simiyu, Manyara, Dodoma na sasa mkoa wa
Njombe.
Alisema
katika mikoa sita migogoro 5,16 imetatuliwa kati ya 4,942 na kufikia wananchi
4,15,000.
Aliwataka
wananchi mkoani hapa kujitokeza kwa wingi ili kupata fursa ya msaada wa kisheri
kupitia kampeni hiyo itakayofanyika kwa muda wa siku 10.
Naye
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo amesema kuwa kupitia
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Wananchi wenye matatizo mbalimbali
ya Kisheria wamefikiwa na kupatiwa huduma za msaada wa kisheria bure na kutatua
changamoto katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Comments
Post a Comment