"MSLAC ITUSAIDIE. KUNA MIGOGORO IMETUSHINDA" – DC KISSA
Hyasinta Kissima – WKS Njombe
Mkuu
wa Wilaya ya Njombe Mhe. Kissa Kasongwa amesema kuwa kupitia Kampeni ya Msaada
wa Kisheria ya Mama Samia katika Wilaya ya Njombe ipo migogoro ya muda
mrefu ambayo imekuwa ikijadiliwa na kuhamishiwa kwa Viongozi mbalimbali lakini
ufumbuzi wa migogoro hiyo umekuwa haupatikani.
Mhe.
Kissa aliyasema hayo Mei 29, 2024 wakati akiwasilisha salamu za Serikali katika
Mkutano wa Baraza la Waheshimiwa Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya
Njombe uliofanyika katika ukumbi wa makao makuu ya Halmashauri yaliyopo Kijiji
cha Kidegembye Kata ya Lupembe Wilayani Njombe.
"Tunaupongeza uongozi wa
Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye chini ya uratibu wa Wizara ya Katiba
na Sheria waliamu kuja na ubunifu wa kuleta huduma za Kisheria za bure Mama
Samia Legal Aid Campaign. Kuna mifupa huko imetushinda Waheshimiwa Madiwani.
Zipo kesi za miaka mingi sana Wananchi wanahamisha malalamiko kwa Viongozi
mbalimbali kila anapokuja Kiongozi mpya kesi zinaanza upya na muafaka
haufikiwi. Mama Samia Legal Aid ipo Wilayani kwetu na leo hii tutaanza na
mgogoro wa Lupembe Saccos ambao naamini huu mfupa hautatushinda."Alisema
Kissa.
Mheshimiwa Kissa amesema kuwa,
mgogoro wa Lupembe Saccos ni kero ambayo inawaumiza Wananchi wengi na wengi
wanaona wanapoteza haki yao kutokana na Wanachama wa Saccos hiyo kuwekeza
mamilioni ya fedha kwa kipindi kirefu na kwa sasa wanapokwenda kuomba fedha zao
Saccos hiyo haina fedha za kuwapatia wanachama wake.
Kwa upande wake Wakili wa
Serikali Mkuu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Candid Nasua amesema kuwa, kupitia
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia timu ya Wataalamu wakiwemo
Wanasheria na Mawakili ipo kwa ajili ya kuhakikisha kila mgogoro unasikilizwa
na kupatiwa ufumbuzi ili haki iweze kutendeka kwa kila anayestahili.
Dhumuni
la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan
ni kuhakikisha kuwa kila mwanachi mwenye nacho na asiyekuwa nacho mwenye
uhitaji wa huduma za kisheria anasaidiwa na anapata haki yake
bila gharama yoyote.
Comments
Post a Comment