MSLAC KUTOA ELIMU MKESHA WA MWENGE – DC MAKETE
Mkuu
wa Wilaya ya Makete Bw. Juma Sweda akiongea na wananchi kwenye mkutano wa
hadhara uliofanyika Kijiji cha Masisiwe Kata ya Ukwama Mei 29, 2024 ikiwa ni
utekelezaji wa MSLAC.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya Makete Bw. William Makufwe akiongea na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Masisiwe Kata ya Ukwama Mei 29, 2024 ikiwa ni utekelezaji wa MSLAC.
Mwanasheria
kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Fredrick Makamba akitoa mada ya sheria kwenye
mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Masisiwe Kata ya Ukwama Mei 29, 2024
ikiwa ni utekelezaji wa MSLAC.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na William Mabusi – WKS
Makete
Mkuu
wa Wilaya ya Makete Bw. Juma Sweda amefurahishwa na utekelezaji wa Kampeni ya
Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inayoendelea kutekelezwa Wilayani humo na
kuwasilisha ombi kwa Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana
ili timu hiyo irudi kutoa elimu siku ya mkesha wa Mwenge utakaofanyika tarehe
18 Juni, 2024 Kata ya Mfumbi.
Mkuu
huyo wa Wilaya ametoa kauli hiyo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji
cha Masisiwe Kata ya Ukwama Mei 29, 2024 alipokwenda kujionea utekelezaji wa
Kampeni hiyo.
“Mie
mwenyewe nimesikiliza elimu inavyotolewa nikasema ewaaa! Nimefurahishwa na
ufundishaji wa Vijana hawa kutoka kwa Waziri Dkt. Pindi Chana dada yetu anayetoka
Ludewa, ambaye naye aliagizwa na Mhe. Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan kuja kutoa elimu ya sheria, kusikiliza kero zenu na kuwashauri. Elimu wanayoitoa naamini
itasaidia kuwapata kutoka miongoni mwenu washauri watakao msaidia Mwenyekiti wenu
wa kijiji kutatatua migogoro,” alisema na kuongeza;
”Elimu
hii itufungue macho kujua je kuna haja ya kuendelea na mgogoro uliokuwepo kati ya
mume na mke, jirani na jirani. Na wakati mwingine unajua mgogoro unaweza kuwa
ni hatua moja tu inagombewa kwenye mpaka. Tarehe 18 Juni, 2024 utafanyika
mkesha wa Mwenge Kata ya Mfumbi, nimeongea na dada yetu Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana
kuiomba timu hii na yeye mwenyewe wawepo kutoa elimu kwa wananchi watakaokuwepo
siku hiyo.”
Naye
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya Makete Bw. William Makufwe ambaye pia
alitembelea timu hiyo amewataka wananchi kuitumia vizuri Kampeni hiyo kwani imekuja
ili wananchi wapate haki yao iliyopotea au kuchelewesha.
Akijibu
swali la Bw. Alfred Masharubu Pira mkazi wa kijiji cha Masisiwe aliyetaka kujua
kama kumpendelea mtoto mmoja kwenye wosia
ni sawa kisheria, Mwanasheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Fredrick
Makamba amesema hakuna shida ilimradi zipo sababu za kufanya hivyo.
“Faida
ya kuandika wosia pamoja na mambo mengine ni kuelekeza mali yako igawanywe vipi
utakapofariki. Aidha, katika kuandika wosia unaruhusiwa kumnyima mwanao wa
kumzaa kurithi mali endapo utakuwa na sababu za kufanya hivyo. Sababu hizo ni
pamoja na kama itagundulika mwanao ameshiriki
tendo la ndoa na mama yake, kutapanya mali, hakuhangaika kukuuguza wakati wa
ugonjwa.” Alisema Bw. Makamba.
Comments
Post a Comment