MSLAC YAWAFUTA MACHOZI WALIOSHINDWA KUMUDU GHARAMA ZA MAWAKILI
Hyasinta Kissima – WKS Njombe
Wananchi wa Kijiji cha
Nundu Kata ya Yakobi Halmashauri ya Mji Njombe wamepongeza ujio
wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kutokana na huduma hiyo
kutolewa bila malipo, ambapo awali Wananchi walidhulumiwa haki zao kutokana na
wengi kushindwa kumudu gharama za Mawakili.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti tofauti mara baada ya timu ya wataalam wa msaada wa kisheria
kufika Kijijini hapo kwa lengo la kutoa elimu, baadhi ya Wananchi wa
kijiji cha Nundu wamesema kuwa, Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
imeendelea kujipambanua kwa kuendelea kuwajali Wananchi, kuwafuta machozi na
kuhakikisha haki inatendeka kwa kila Mtanzania bila kujali kipato cha
chake.
"Wakati mwingine katika
kudai haki inaweza kufikia hatua unakua haujaridhika na haujui uende wapi. Unaweza
kuwa umeingia kwenye mgogoro na mtu mwenye uwezo wa kuwa na Mawakili au
taasisi ambayo wapo Wanasheria hivyo unafikia hatua unakosa msaada na haki
inapotea. Msaada wa Kisheria wa Mama Samia sisi walala hoi tunaona mwanga"
Alisema Innocent Mlange mkazi wa Kijiji cha Nundu.
Bernard Isdory ni mkazi wa
Kijiji cha Nundu ambaye yeye aliambatana na shemeji yake (mke wa mdogo
wake) akilalamika kuhusu mdogo wake kumtelekeza mkewe na watoto
wawili na kuwafukuza katika nyumba waliokuwa wamejenga na kuishi pamoja awali
na kwenda kuishi katika Mkoa wa Ruvuma.
Bernard anasema kuwa mara baada ya kuonana na wataalam waliofika kijijini hapo kupitia kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, imewajengea uwezo wa namna ya kuendelea na shauri hilo na matarajio yao ni kuona mgogoro huo unafikia muafaka na haki kutendeka.
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imeendelea kuwafikia Wananchi katika Kata na Vijiji mbalimbali vya Mkoa wa Njombe ambapo Wananchi mbalimbali wameendelea kujitokeza kuchangamkia fursa hiyo.
Comments
Post a Comment