SAGINI AITAKA TUME YA HAKI ZA BINADAMU KUTOA ELIMU JUU YA HAKI YA KUJIELEZA
Na Yasinta Kissima – WKS
Dodoma
Naibu
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini ameitaka Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora kujipambanua katika majukumu yao na kutambua
kazi inayofanywa na Serikali katika kutetea Haki za Binadamu na kuangazia
baadhi ya watu wanaovuruga na kukashifu haki za wengine wakiwemo Viongozi
kwa sababu ya uwepo wa uhuru wa kujieleza.
Naibu
Waziri Sagini ameyasema hayo Mei 8, 2024 katika Makao Makuu ya Tume maeneo ya Kilimani
jijini Dodoma ikiwa ni mwanzo wa ziara yake ya kuzitembelea Taasisi
zilizopo chini ya Wizara hiyo kwa lengo la kujifunza na kufahamu majukumu yao
katika kufanikisha kazi za Wizara.
"Jukumu
la Tume ni kuangalia kwa kiwango gani haki za Binadamu na Utawala Bora
zinatekelezwa na Taasisi mbalimbali za Umma au hata watu binafsi katika
majukumu yao. Yapo mambo mengi ambayo Serikali imefanya yanayogusa haki za
Binadamu lakini je katika ripoti zinazoandikwa na Tume hayo yameripotiwa?"
Alihoji Mhe. Sagini
Aliendelea
kusema, "Serikali ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan imefanya maamuzi magumu
kufanya elimu ya msingi kuwa miaka kumi, utoaji wa elimu bila malipo mpaka
kidato cha sita, ujenzi wa Zahanati na Hospitali katika maeneo mbalimbali.
Kwenye Demokrasia imetoa uhuru wa watu kutekeleza majukumu yao ya kisiasa
yote haya yanalenga kulinda Haki za Binadamu. Lakini wanaibuka watu na
lugha za kejeli, lugha za matusi na lugha za kufedhehesha Viongozi wetu, Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iangalie na kujitokeza hadharani kuelimisha
watu juu ya yale wanayoyaona na yale yanayotendwa na Watanzania." Alisema
Naibu Waziri.
Aidha,
Sagini ameitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuboresha mahusiano na
ushirikiano mahali pa kazi ili kuleta mafanikio na ufanisi katika
kutimiza malengo ya Taasisi.
Comments
Post a Comment