SERIKALI KUENDELEA KUKISAIDIA CHAMA CHA MSALABA MWEKUNDU
Waziri
wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi
Dkt. Pindi Chana (katikati), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi
wa Umma na Utawala Bora Zanzibar Mhe. Haroun Ali Suleiman (kushoto), Naibu
Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile (kulia) wakisubiri kuanza kwa Maadhimisho
ya Miaka 62 ya Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania, Mei 11, 2024 Jijini Dodoma.
Naibu
Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Dotto Biteko akikagua mabanda ya Maonesho kwenye
Maadhimisho ya Miaka 62 ya Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania, Mei 11, 2024
Jijini Dodoma. Kushoto kwake ni Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana.
Na William Mabusi – WKS Dodoma
Naibu
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dotto Biteko na Waziri wa
Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana wamesema Serikali itaendelea kukiwezesha
Chama cha Msalaba Mwekundu nchini kutoa huduma za uokozi kwa wananchi
wanaopatwa na madhira ama changamoto mbalimbali zinazoathiri maisha yao.
Kauli
hiyo imetolewa kwa nyakati tofauti wakati viongozi hao wakihutubia kwenye
kilele cha Maadhimisho ya miaka 62 ya Chama cha Msalaba Mwekundu nchini Mei 11,
2024 Jijini Dodoma.
Maadhimisho
hayo yamefanyika Kitaifa katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete na kuhudhuriwa na
mamia ya wanachama wa Taasisi hiyo kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na
Zanzibar yakibeba kauli mbiu isemaya “Natoa kwa furaha na furaha ninayotoa ni
zawadi.”
“Ninyi
huwa mstari wa mbele na kuhatarisha uhai wenu kwa kuokoa maisha ya watu wengine,
kwa kufanya hivyo mnaisaidia Serikali katika utoaji wa huduma za kibinadamu kwa
wahanga wa majanga mbalimbali, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Red Cross
katika mazingira yote hata ya furaha.” Amesema Dkt. Biteko huku akimtaka Rais
wa Chama cha Msalaba Mwekundu nchini Mhe. David Kihenzile kuendelea kuwasajili
vijana kuongeza wanachama kwenye Chama hicho.
Naye
Dkt. Chana akiongea kwenye maadhimisho hayo amesema ”Wizara itaendelea kuweka
kanuni na miongozo mbalimbali kuhakikisha Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania kinatimiza
majukumu yake nchini. Aidha, Serikali itaendelea
kufanya kazi kwa karibu na Red Cross kuhakikisha Wananchi wanaopatwa na madhira
na changamoto mbalimbali zinazoathiri maisha yao wanahudumiwa kwa wakati.”
Awali
akimkaribisha Mgeni Rasmi Rais wa Chama cha Msalaba Mwekundu nchini na Naibu Waziri
wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile amesema kwa sasa Red Cross ina Matawi 1600
Tanzania Bara na Zanzibar ikiwa na wanachama zaidi ya laki 6. Aidha, aliongeza
kuwa Red Cross imo mbioni kujenga ofisi mpya kwenye mikoa 12 na kwamba ina
mpango wa kujenga nyumba 35 kwa Watanzania waliobomolewa nyumba zao Wilayani
Hanang’.
Comments
Post a Comment