DC NJOMBE AWATAKA WANANCHI KURIPOTI MIGOGORO KWA MSLAC
Mkuu wa Wilaya ya Njombe Mhe. Kissa Kasongwa akipokea
nakala ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vipeperushi
kutoka kwa Wakili wa Serikali Mkuu Candid Nasua mara baada ya kutembelea banda
la Wizara ya Katiba na Sheria Mei 31, 2024.
Huduma ya msaada wa Kisheria ikiendelea kutolewa katika
banda la Wizara ya Katiba na Sheria ambapo Bi. Edith Shekidele, Wakili wa
Serikali akitoa huduma ya Msaada wa Kisheria kwa mwananchi aitwae Leonard
Hongoli.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Hyasinta
Kissima – WKS Njombe
Mkuu wa Wilaya ya Njombe Mhe.
Kissa Kasongwa amewataka Wananchi wa Wilaya ya Njombe kuhakikisha wanatumia
uwepo wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kutatua migogoro ya
kisheria ambayo walikuwa wakiifikisha kwa viongozi hao na haikuweza
kufikia muafaka.
Mheshimiwa Kissa ameyasema hayo Mei
31, 2024 wakati alipotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria kwa
lengo la kukagua shughuli zinazoendelea na kuzungumza na Wananchi waliokuwa
wakipatiwa huduma mbalimbali za Kisheria katika banda hilo.
"Tunamshukuru Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwani kupitia kampeni hii tumeanza kuona matokeo yake. Mfano
tulikuwa na mgogoro wa Wananchi wa Lupembe Saccos lakini mpaka ninavyozungumza
Madalali wapo kazini kukusanya madeni kwa waliokopeshwa kupitia Saccos na fedha
hazijarudishwa."Alisema Kissa.
Aliendelea
kusema "Niwaombe Wananchi wa Njombe kuhakikisha mnatumia kampeni ya Msaada
wa Kisheria kutatua migogoro ya Kisheria ambayo mlikuwa mnaiwasilisha Ofisini. Wapo
Mawakili na Wataalamu wa Sheria hapa na huduma hizi ni bure. Watawashauri
na kama mtahitaji Mawakili mtapatiwa bure."
Kwa upande wao baadhi ya Wananchi waliopatiwa huduma za Kisheria katika banda la Wizara na Wataalamu wa sekta hiyo akiwemo Leonard Hongoli wamesema kuwa ipo migogoro ambayo ilikuwa ikiwakabili lakini mara baada ya kuwasilisha maelezo ya migogoro hiyo kwa Wataalamu wa Sheria wameweza kuelekezwa ni hatua gani za kufuata ili kuweza kuleta suluhu.
Comments
Post a Comment