JAMII IELIMISHWE JUU YA USULUHISHI NJE YA MAHAKAMA - JAJI MKUU
Hyasinta
Kissima - WKS
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.
Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema kuwa ni vyema Wizara ya Katiba na Sheria
kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ikaendelea kutoa elimu kwa
jamii kuhusu faida za kufanya usuluhishi wa migogoro nje ya Mahakama ili kuepuka
kutumia muda mrefu kusikiliza Mashauri, kuepuka gharama kwa
wanaohusika katika migogoro (Wadaawa) na kuepuka msongamano wa
Mashauri Mahakamani.
Profesa Ibrahim alisema hayo
katika mazungumzo na Naibu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria
Mhe. Jumanne Sagini wakati alipomtembelea Jaji Mkuu katika Ofisi za
Mahakama ya Rufani Kivukoni Jijini Dar es Salaam Juni 20,2024 kwa lengo la
kufahamu majukumu na muundo wa Muhimili wa Mahakama, Kuimarisha mashirikiano
baina ya Wizara na Muhimili na kujifunza namna walivyoweza kufanikiwa kwenye
masuala ya miradi ya maendeleo na matumizi ya TEHAMA.
“Katiba ya Tanzania katika
kipengele cha utoaji haki, inasisitiza katika kukuza na kuendeleza
usuluhishi baina ya wanaohusika katika migogoro. Suala la kusuluhishwa kwa
dakika thelathini linaweza kuchukua miaka zaidi ya kumi. Zipo baadhi ya Nchi
ambazo zaidi ya asilimia tisini na tano (95%) ya Mashauri yanaisha kwa njia ya
Usuluhishi. Ni vyema Sheria ielekeze kuwa, kabla ya suala kwenda Mahakamani
lianze kwenye Usuluhishi kwani kunajenga ukaribi na sio uadui.” Alisema Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma.
Kwa upande wake Naibu Waziri
wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini ameupongeza Muhimili wa
Mahakama kwa kazi kubwa wanazofanya katika kusimamia utoaji haki kwa Wananchi,
kusimamia ujenzi wa Mahakama katika maeneo mbalimbali Nchini na pia kufanya
mageuzi katika utendaji wa Mahakama ikienda sambamba na matumizi ya TEHAMA.
Katika mazungumzo hayo,
Naibu Waziri Sagini amesema katika kipindi cha nyuma cha utendaji kazi kama
Katibu Tawala, kulikuwa na changamoto ya Kamati ya Maadili ya Mahakimu
katika ngazi za Wilaya na Mikoa kutokutana na kufanya vikao na limekuwa
likisahaulika ambapo Jaji Mkuu amesema kuwa kwa sasa Kamati hiyo ikiwa na
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama imekuwa ikizunguka katika Mikoa
mbalimbali Nchini kwa lengo la kuzijulisha Kamati za Wilaya na
Mikoa namna ambavyo zinatakiwa kufanya kazi na kuzijengea uwezo zaidi.
Kikao hicho kilihudhuriwa na
Msajili Mkuu wa Mahakama Mhe. Eva Kiaki Nkya, Msajili wa Mahakama ya Rufani
Mhe. George Hillary Herbet, Naibu Msajili Mahakama Kuu Mhe. Venance Mlingi
ambaye pia ni Katibu wa Jaji Mkuu wa Tanzania na Mhe. Hakimu Mkazi Jovine
Constatine ambaye pia ni Katibu wa Msajili Mkuu wa Mahakama.
Comments
Post a Comment