KUNA SULUHISHO LA KERO ZENU NDANI YA SERIKALI – MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI
Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akimsikiliza Mwenyekiti wa Umoja wa
Wataafu Tanzania wanaolipwa na Hazina mzee John Joseph Kanyeto akitoa kero yake
kabla ya kuzindua Kliniki ya sheria, Juni 26, 2024 Viwanja vya Mwalimu Nyerere,
Dodoma.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
William
Mabusi – WKS Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewahakikishia wananchi kuwa Serikali
imejipanga kuhakikisha inatatua kero na changamoto zao katika kuimarisha
utengamano na utulivu nchini.
Dkt. Feleshi ameyasema hayo
alipokuwa anazindua Kliniki ya kutoa ushauri na elimu ya sheria iliyoandaliwa
na Ofisi yake, tarehe Juni 26, 2024 Viwanja vya Mwalimu Nyerere Jijini Dodoma.
Kliniki hiyo itafanyika kwa wiki nzima kuanzia leo Juni 26 hadi Julai 03, 2024.
“Kliniki hii na zingine
zitakazoendelea kuratibiwa na Serikali zimelenga kutoa suluhisho ya kero zenu, kumwezesha
mwananchi kupata huduma bora kwa wakati na kuongeza utengamano na utulivu na
hivyo kuchochea maendeleo ya jamii. Mahala pasipokuwa na masikilizano na kuwepo
namna ya kujadili changamoto au kero mara nyingi kunakuwa na fukuto ambalo
hupelekea maendeleo yasifikiwe kwa wakati lakini pia husababisha uadui kwani
miongoni mwa pande zilizo katika mgogoro hupoteza mali, haki na hata maisha.” Alisema.
Ametoa rai kwa Mawakili wa Serikali na Wadau wote wa sheria, “ili
kujitofautisha na majukwaa mengine sisi wajibu wetu ni kutatua kero siyo
kupapasa, Wadau wote wa sheria lengo letu ni kushughulikia kero za wananchi na
si kuwaacha waangukie mikononi mwa watu wengine wasio wataalam na mwisho wa
yote hawawezi kutatua kero zao kwa ukamilifu.”
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali amesema uanzishwaji wa Kliniki za sheria ni kutekeleza maelekezo ya Katiba
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwatumikia wananchi lakini pia ni utiifu wa
kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo amekuwa
akiyatoa kwenye hotuba zake akikumbusha viongozi kushughulikia kero za wananchi
kwa wakati. Migogoro isiposhughulikiwa kwa wakati itaishia kwenda mahakamani
ambako kuna gharama ya muda, gharama za ushindani kwa sababu mahakamani ni
pande mbili zinapigania haki.
Awali akitoa salaam katika
hafla hiyo kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na
Sheria Bi. Mary Makondo amesema kupitia Sheria ya Huduma ya Msaada wa Kisheria
wananchi wameendelea kuangaliwa kwa jicho la pekee katika mageuzi yanayofanywa nchini
ya kuboresha huduma za sheria kwa kuzisogeza karibu zaidi na waliko wananchi ili
kero zao ziweze kutatuliwa kwa wakati.
Ameshukuru Wadau walioitika
wito kushiriki katika Kliniki hiyo kutatua kero za wananchi kwa haraka akizitaja
kwa uchache Wizara ya Ardhi, Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. “Sisi sote tumewekwa kwa lengo la
kuwasasidia wananchi kwa dhamana ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kitu ambacho tunapaswa kuendelea kukifanya kwa vitendo.” Alisema.
Aidha, Bi. Makondo ameshukuru
Serikali kwa kuendelea kuiwezesha Wizara na Taasisi zake katika kutekeleza
majukumu mbalimbali ya kuwatumikia wananchi. Akitumia mfano wa Kampeni ya Msaada
wa Sheria ya Mama Samia amesema Wizara kwa kushirikiana na Wadau wa haki imeendelea
kutatua kero nyingi kwa wananchi hususan wa hali ya chini.
Vile vile, Bi. Makondo amesema Wizara imeendelea kuboresha
mifumo mbalimbali ya TEHAMA ikiwemo mfumo wa Usajili Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria
na kuanzisha Kituo cha kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kwa njia ya simu -
Call centre.
Comments
Post a Comment