MWENYEKITI WA CCM WILAYA YA MAKETE ASISITIZA MATUMIZI YA KISWAHILI MAHAKAMANI
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya
Makete Ndg. Clement Ngajilo akiongea na wananchi wa kijiji cha Ipelele Kata ya
Ipelele kwenye Mkutano wa Kampeni ya Mama Samia, Juni 2, 2024 Makete.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya
Makete Ndg. Clement Ngajilo (wa pili kulia) akisikiliza mada zilizokuwa zinatolewa
wakati wa mkutano wa Kampeni ya Mama Samia uliofanyika kijiji cha Ipelele Kata
ya Ipelele, Juni 2, 2024 Makete.
Wakili wa Serikali kutoka
Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Zakaria Mzese (kushoto) akitoa huduma ya msaada
wa kisheria kwa mkazi wa kijiji cha Ipelele, Juni 2, 2024 Makete.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxx
William
Mabusi – WKS Makete
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya
Makete Ndg. Clement Ngajilo ameiomba Serikali kutumia lugha ya Kiswahili kwenye
Mahakama ili lugha isiwe kikwazo kwa wananchi kupata haki zao.
Ndg. Ngajilo ameyasema hayo
kwenye mkutano wa hadhara wakati wa kutekeleza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya
Mamam Samia uliokuwa unafanyika kijiji cha Ipelele Kata ya Ipelele Juni 2, 2024
Wilayani Makete.
“Wananchi wengi hawana uwelewa
wa lugha za Mahakama na wanapopeleka kesi zao mahakamani hususan kwenye ngazi za
juu zinazohitaji uwakilishi lugha inayotumika kwa sehemu kubwa huwa kikwazo hali
inayopelekea wananchi kupoteza haki zao. Naomba sheria hizo kuboreshwa na
itumike lugha mama yaani Kiswahili ili hata mwananchi asiye na uwezo wa kumsimamisha
Wakili kutokana na changamoto ya rasilimali fedha aweze kusimama mwenyewe.”
Alisema.
Akiongelea kuhusu hifadhi ya
barabara yaani road reserve amesema kwa
baadhi ya maeneo Serikali ilipima vipimo hivyo muda mrefu bila kuyatumia na
kama wananchi hawajui juu ya vipimo vilivyopimwa huamua kufanya shughuli zao, baadaye
Serikali inapotaka kuyatumia maeneo hayo wananchi wanaambiwa kuwa wameingia
kwenye hifadhi ya barabara na kuambiwa watoke bila fidia, mwananchi anaanza
kuona kero, hivyo ni busara Serikali kwa nyakati tofauti iwe na utamaduni wa
kutoa elimu kwa wananchi kuwa ndani ya eneo la mita kadhaa hawaruhusiwi kujenga
au kufanya shughuli zote za kibinadamu kuepusha usumbufu unaojitokeza.
Bw. Ngajilo amesema kwa vijiji
ambavyo havikupitiwa na Kampeni wananchi wana haki ya kupeleka changamoto kwenye
ofisi za Halmashauri zao na kuwaagiza watumishi wa Halmashauri wanaoshiriki
kwenye Kampeni hiyo kutumia elimu waliyopata wakati wa maandalizi na hatimaye uzoefu
wakati wa utekelezaji wa kampeni hiyo kuendelea kutatua kero za wananchi.
Mwisho wa hotuba yake ameshukuru
Serikali kwa kutenga muda wa kutoa elimu ya sheria kwa jamii kwani jamii huko
vijijini ina migogoro mingi na kwamba wana Makete ne wana Njombe wameipokea
kampeni hiyo kwa mikono miwili akiomba iwe endelevu pale inapowezekana ili
kuwaondolea shida wananchi.
Akiongea kwenye mkutano huo Bw. Omega Frank Fungo mkazi wa Kijiji cha Ipelele amesema “ni uamuzi mzuri kwa kiongozi wa nchi kutuma Wizara kusikiliza kero za wananchi, kuna sehemu nyingi hatukujua haki zetu lakini sasa tunajua na tutafanyia kazi elimu tuliyopata, sasa Ipelele mambo safi.”
Comments
Post a Comment