WANANCHI MAKETE WAIFAGILIA MSLAC
William
Mabusi – WKS Makete
Wananchi Wilayani Makete
wamesema Kampeni ya Msaaada wa Kisheria ya Mama Samia imewapa elimu ya kutosha kuwaepusha
na migororo, wakati huo huo imewasaidia pakubwa kutatua migogoro waliyokuwa
nayo.
Wananchi hao wametoa kauli
hiyo kwa nyakati tofauti wakati wa mikutano ya hadhara ya kutekeleza Kampeni
hiyo Wilayani humo.
Bw. Amos Tweve mkazi wa kijiji
cha Nkenja Kata ya Kitulo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo
Juni 04, 2024 amesema “mtafikiri mlinusa kijiji hiki kina shida fulani mkaona mpeleke
watu wenye taaluma hii waje kufundisha hiki mlichofundisha, naombeni elimu hii
muifikishe kwa wantanzania wengine.”
Katika mkutano huo Bw. Daudi
Kinga alisema “nyie hamjui tu ila kwa elimu hii kuna migogoro mingi mmeitatua,
Mungu awabariki sana, nawaomba wananchi wenzangu twende tutekeleze
waliyotwambia wataalam.”
Katika hatua nyingine Bi. Rose
Mbogela mkazi wa kijiji cha Matamba Kata ya Matamba kwenye mkutano wa kampeni
hiyo uliofanyika Juni 3, 2024 anasema hakujua afanye nini baada ya mume wake
kufariki na eneo aliloishi na mume wake kuvamiwa na mtu akidai ni mali yake.
Kitu cha kusikitisha zaidi ni pale ambapo Baraza la Ardhi la Kata lilipotoa
hukumu iliyomnyima haki Bi. Mbogela kitu ambacho ni kinyume na sheria kwani
Mabaraza ya Ardhi ya Kata hayatakiwi kutoa hukumu baada ya marekebisho ya
sheria mwaka 2021. Hukumu hiyo ilitupiliwa mbali na Baraza la Ardhi na Nyumba
la Wilaya ya Makete mwaka jana. Baada ya hukumu hiyo kutupiliwa mbali bado Bi.
Mbogela amekuwa akiishi kwa vitisho, Timu ya MSLAC imemhakikishia Bi. Mbogela
kwamba atabaki kuwa mmiliki wa eno hilo na endapo huyo mvamizi ataendelea
kumsumbua awasiliane na Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete.
Kampeni hiyo ilikuwa
inafanyika katika Halmashauri zote sita za Mkoa wa Njombe baada ya kuzinduliwa
na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Doto Biteko
Mei 26, 2024 imekamilika leo Juni 4, 2024.
Comments
Post a Comment