WANANCHI MAKETE WALALAMIKIA FIDIA UHARIBIFU WA WANYAMAPORI
Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka Wizara ya Katiba na
Sheria Bw. Richard Jacopio akiwasilisha mada ya sheria kwenye mkutano wa
hadhara uliofanyika kijiji cha Ivalalila Kata ya Iwawa, Mei 31, 2024 Makete.
Afisa Wanyamapori kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Bw. Francis Malembo akiwasilisha mada ya Sheria ya uhifadhi wa wanyamapori kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Ivalalila Kata ya Iwawa, Mei 31, 2024 Makete.
Afisa Msajili Msaidizi RITA Wilaya ya Kyela Bi. Nenduvotho
Loy akiwasilisha mada ya Wosia, Mirathi, Usajili wa Vizazi na Vifo kwenye
mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Ivalalila Kata ya Iwawa, Mei
31, 2024 Makete.
xxxxxxxxxxxxxxxxx
William
Mabusi – WKS Makete
Wananchi Wilayani Makete
wameiomba Serikali kuongeza fidia inayotolewa kwa wananchi wanaojeruhiwa au
kupata ulemavu wa kudumu, familia iliyopoteza ndugu kwa kuuliwa au kuharibiwa
mazao na wanyamapori, kwani kiwango cha sasa hakikidhi uharibifu wa wanyamapori
hao.
Malalamiko hayo yametolewa na
wananchi wa kijiji cha Ivalalila Kata ya Iwawa Halmashauri ya Wilaya ya Makete
Mei 31, 2024 kwenye Mkutano wa hadhara baada ya mada mbalimbali kutolewa
ikiwemo ya Sheria ya uhifadhi wa wanyamapori ikiwa ni utekelezaji wa kampeni ya
kutoa huduma ya msaada wa kisheria ya Mama Samia inayoendelea kutekelezwa
kwenye Halmashauri zote Sita mkoani Njombe.
Bw. Amua Mahenge mkazi wa
kijiji cha Ivalalila alisema, ”fidia ya uharibifu wa Wanyamapori ni ndogo
ukilinganisha na gharama tunazoingia wakulima wakati wa kilimo. Kwa mfano
kwenye heka moja tunatumia mifuko mitatu ya mbolea yenye thamani ya zaidi ya
shilingi elfu sabini na nne (74,000/-) kwa mfuko mmoja sawa na shilingi 222,000
na hiyo ni gharama ya mbolea tu, halafu
fidia ya Serikali ni sh 100,000 kwa heka iliyoharibiwa na wanyamapori.”
Aidha, wananchi hao walionesha
kutoridhishwa kwao kwa fidia ya shilingi laki tano kwa mtu aliyejeruhiwa na
mnyamapori na kusababishiwa ulemavu wa kudumu, ila mtu akithibitika kamuua
mnyama hukumu yake ni kifungo cha miaka isiyopungua ishirini na isiyozidi thelathini.
Akijibu swali hilo, Afisa
Wanyamapori kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) Bw. Francis
Malembo amesema viwango vya fidia kutokana na uharibifu wa wanyamapori
vimelalamikiwa hata maeneo mengine na Serikali inafanyia kazi marekebisho ya
viwango vya fidia, ingawa kwa sasa viwango vya zamani vya kifuta machozi na
jasho vya mwaka 2011 vitaendelea kutumika.
Naye Bw. Nowadi Mbilinyi mkazi wa Ivalalila akichangia mada hiyo ameomba TAWA kuruhusu njia ya mkato kwa wananchi kutoka Ivalalila kwenda Kigala Kata ya Kigala kupitia Pori la akiba la Mpanga Kipengele kwani pori hilo halina wanyama wakali wa kudhuru binadamu.
Comments
Post a Comment