HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA ZINAPATIKANA SABASABA BILA MALIPO
Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Jumanne Sagini (kushoto) akimsikiliza Wakili wa Serikali
Mkuu Candid Nasua kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, akimpa
tathmini kuhusu hali ya utoaji wa huduma za Kisheria na huduma mbalimbali
kwa Wananchi wanaotembelea banda hilo. Julai 5, 2024 Dar es Salaam.
Baadhi ya Wananchi wakiwa
katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria kwa ajili ya kupata huduma
mbalimbali kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) Julai 5,
2024 jijini Dar es Salaam.
xxxxxxxxxxxxxx
Hyasinta
Kissima – WKS Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Jumanne Sagini ametaka Wananchi wanaofika katika Maonesho ya 48 ya
Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) kutembelea katika banda la Wizara ya Katiba na
Sheria ili kutapa huduma mbalimbali
ikiwemo Msaada wa Kisheria.
Naibu Waziri Sagini
ameyasema hayo Julai 5, 2024 jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea
banda la Wizara kuangalia hali ya upatikanaji wa huduma hizo kwa Wananchi wanaotembelea banda hilo.
"Wapo Wananchi wanatoka
katika maeneo mbalimbali Nchini na wengi kutokea jijini Dar es Salaam na
wanahitaji msaada wa kisheria. Niwasihi sana kufika katika banda la Wizara ya
Katiba na Sheria na kupata huduma hizi bure. Wizara imejizatiti kuhakikisha
kuwa kila Mwananchi atakayetembelea katika banda na mwenye shida atapata
huduma. Wapo Mawakili wa Serikali, Wanasheria wenye weledi na ambao wapo
tayari kuhakisha kuwa haki kwa kila Mtanzania inatendeka." Alisema Naibu
Waziri Sagini.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti tofauti, baadhi ya Wananchi waliofika katika banda la Wizara ya
Katiba na Sheria akiwemo Johnson Msemwa na Katarina Mpangilye
wameonesha kufurahishwa na uwepo wa huduma hizo viwanjani hapo jambo ambalo
limewawezesha kupata ushauri kuhusu masuala ya kisheria yaliyokuwa
yakiwakabili.
“Nilikuwa nina changamoto
kuhusu malezi ya watoto mara baada ya kutengana na mzazi mwenzangu. Nimefika
katika banda hili la Katiba na Sheria nimepata elimu ya kutosha na Wataalamu wamenisaidia
kufanya mawasiliano na mzazi mwenzangu na kupanga namna ya kuweza kufikisha
huduma za matunzo kwa watoto.” Alisema mama mmoja ambaye hakupenda jina lake
litajwe.
Kwa upande wake Kaimu
Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba
na Sheria Bi. Ester Msambazi amesema kuwa mpaka sasa Kampeni hiyo imeshafika
katika mikoa 7 na kufikia zaidi ya Wananchi 495,000 wakiwemo
Wanawake, Wanaume na Watoto na wengi wamenufaika kwa kupata elimu, ushauri na
utatuzi wa migogoro yao.
Wizara ya Katiba na Sheria
katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara itaendelea kutoa huduma
mbalimbali na kutatua changamoto mbalimbali za Wananchi ikiwemo migogoro ya
Ardhi, Ndoa, Mirathi, ukatili wa kijinsia.
Comments
Post a Comment