KAMATI YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA PROGRAMU YA KIZAZI CHENYE USAWA

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu utekelezaji wa Programu ya Kizazi Chenye Usawa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angella Kairuki akiongea kwenye kikao cha Kamati hiyo na Menejimenti ya Wizara ya Katiba na Sheria, Julai 11, 2024 Mtumba, Dodoma.

Kaimu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Sera na Mipango Bw. Mbaraka Stambuli akichangia hoja kwenye kikao cha Menejimenti ya Wizara ya Katiba na Sheria na Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu utekelezaji wa Programu ya Kizazi Chenye Usawa, Julai 11, 2024 Mtumba, Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara ya Haki za Binadamu Bi. Nkasori Sarakikya akiwasilisha taarifa ya Wizara juu ya jitihada zake za kuwezesha wanawake katika kufikia kizazi chenye usawa, Julai 11, 2024 Mtumba, Dodoma.

Sehemu ya wajumbe wa Menejimenti ya Wizara kwenye kikao na Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu utekelezaji wa Programu ya Kizazi Chenye Usawa, Julai 11, 2024 Mtumba, Dodoma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu utekelezaji wa Programu ya Kizazi Chenye Usawa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angella Kairuki (katikati) kwenye picha ya pamoja na Menejimenti ya Wizara ya Katiba na Sheria, Julai 11, 2024 Mtumba, Dodoma.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

William Mabusi – WyKS Dodoma

Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu utekelezaji wa Programu ya Kizazi chenye usawa inayoongozwa na Mwenyekiti Mhe. Angella Kairuki ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa jinsi inavyotekeleza maeneo ya usimamizi wa haki na kuwezesha nchi kutekeleza programu ya kizazi chenye usawa.

Pongezi hizo amezitoa kwenye kikao cha Kamati hiyo na Menejimenti ya Wizara ya Katiba na Sheria cha kupokea taarifa ya Wizara juu ya jitihada zake za kuwezesha wanawake katika kufikia kizazi chenye usawa, Julai 11, 2024 Jijini Dodoma.

“Maeneo mbalimbali mnayotekeleza kama kukabiliana na unyanyasaji na ukatili wa kijinsia na watoto, jitihada za kugusa makundi maalum katika utoaji haki, usawa wa uchumi kwa ujumla yanapelekea nchi kuwa na kizazi chenye usawa.” Alisema baada ya Wizara kuwasilisha taarifa juu ya juhudi za kutekeleza mipango na programu za Serikali za kukuza na kulinda haki za wanawake ikiwa ni pamoja na Programu wa Kizazi Chenye Usawa (Generation Equality Forum-GEF).

Mhe. Kairuki amehimiza usajili wa Watoa huduma ya msaada wa kisheria ili kuongeza idadi yao kuwezesha kuwafikia wahitaji wengi zaidi wanaokosa utetezi wa kisheria, huku akiitaka pia Wizara kuongeza uhamasishaji wa kutafuta rasilimali fedha kutoka kwa wadau mbalimbali kupata fedha zaidi za kutekeleza kampeni hiyo.

Akiwasilisha taarifa hiyo Mkurugenzi wa Haki za Binadamu Bi. Nkasori Sarakikya amesema Wizara imekuwa ikitekeleza Programu ya Kizazi Chenye Usawa kwa kuwa na sheria zinazolinda haki za wanawake kama Sheria ya Ndoa Sura ya 29, Sheria ya Msaada wa Kisheria Sura ya 21, Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusu Umiliki wa Utajiri na Maliasilia za Nchi Sura ya 449 miongoni mwa zingine na Kampeni ya msaada wa sheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign).

 Aidha, mwaka 2023 Wizara iliunda Jukwaa la Kitaifa la Haki Mwanamke (Women Justice Forum) kuunganisha jitihada za wadau mbalimbali katika kushughulikia masuala au changamoto zinazowakabili wanawake katika mnyororo wa upatikanaji haki hapa nchini hususan masuala ya ukatili dhidi ya wanawake, huduma za msaada wa kisheria na ulinzi wa haki za wanawake kwa ujumla.

Akichangia katika kikao hicho Kaimu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Sera na Mipango Bw. Mbaraka Stambuli amesema baada ya Kampeni hiyo kutekelezwa mikoa saba imeonekana kuna uhitaji mkubwa wa msaada wa kisheria kwa kwananchi na hivyo Wizara imeongeza mara tatu bajeti ya kutekeleza Kampeni hiyo kutoa shilingi bilioni mbili kwenye bajeti ya 2023/24 na kuwa shilingi bilioni sita kwa bajeti ya mwaka 2024/25.

 Kuundwa kwa Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa ni mwendelezo wa kutekeleza maazimio ya Mkutano wa Beijing kuhakikisha kwamba ulimwenguni kunakuwa na kizazi chenye usawa. Ili kufikia azma hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mwaka 2021 aliunda Kamati ya Kitaifa ya Ushauri Kuhusu Utekelezaji wa Programu ya Kizazi Chenye Usawa kufuatilia utekelezaji wake na kumshauri. Kamati hiyo inamaliza muda wake mwaka 2026.






Comments

Popular posts from this blog

USAJILI WA VIZAZI NA VIFO NI TAKWA LA KISHERIA

UONGOZI WA MAHAKAMA YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU NA WATU YAKUTANA NA VIONGOZI WA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA

BODI YA KITAIFA YA USHAURI YA MSAADA WA KISHERIA YATEMBELEA WASAIDIZI WA KISHERIA IRINGA