SAGINI AIPONGEZA MAHAKAMA KWA MSHIKAMANO
Baadhi ya Wananchi, ndugu,
jamaa na marafiki walioshiriki katika dua ya kumwombea Amina Nyanda Juma ambaye
ni mama mzazi wa Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof Ibrahim Juma ambaye alizikwa
Juni Mosi, 2024 Tarime mkoani Mara
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Hyasinta
Kissima - WKS
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini
ameipongeza Mahakama kwa maboresho makubwa yaliyofanyika katika utendaji kazi,
majengo, matumizi ya TEHAMA, na kwa namna wanavyoshikamana na kuonesha
upendo katika masuala mbalimbali ya
kijamii ikiwemo misiba.
Naibu Waziri Sagini
ameyasema hayo Julai 7, 2024 Tarime mkoani Mara wakati aliposhiriki katika dua
maalumu ya kumwombea marehemu Amina Nyanda Juma ambaye ni mama mzazi wa
Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof Ibrahim Juma ambaye alizikwa Juni Mosi, 2024,
mkoani humo.
"Niwapongeze sana
Mahakama kwa namna mlivyoshiriki toka mlipopokea taarifa za msiba, katika
kipindi cha mazishi na leo katika arobaini ya Mama yetu. Namwona Mtendaji Mkuu
wa Mahakama, Waheshimiwa Majaji wa Mahakama za Rufani na Mahakama Kuu, Mke wa
Jaji Mstaafu Mama Chande, Watumishi mbalimbali wa Mahakama hakika mmeonesha
mshikamano na upendo katika kufanikisha haya yote. Unapoona mshikamano huu ujue
yupo mtu ambaye yupo nyuma ya mafanikio haya na anatuunganisha sote na huyu ni
Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Juma hivyo hatuna budi kumfariji yeye na familia yake
na kushiriki katika dua hii." Alisema Sagini.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama
Prof. Elisante Ole Gabriel akiwasilisha salamu za shukrani kwa niaba ya Jaji
Mkuu amesema kuwa neno pekee analoweza kusema ni asante kwa yale
yote yaliyofanyika katika kipindi chote cha msiba na Mwenyezi Mungu aendelee
kuwabariki na kudumisha umoja huo.
Kadhalika, Prof. Elisante ameelezea kuwa, Wananchi wa Tarime wanapaswa kujiona kuwa nao ni sehemu ya Mahakama na kujivunia mafanikio ya Mahakama ambapo kwa sasa Mahakama inaendelea kufanya maboresho mengi na ni vyema wakayafahamu na kunufaika na matunda ya maboresho ya Mahakama ikiwemo kutumia mfumo wa kupata mrejesho na kupata huduma kuhusu masuala ya Mahakama kwa kupiga namba 0752500400 bila malipo.
Comments
Post a Comment