SAGINI AKOSHWA NA UBUNIFU WA MAHAKAMA KATIKA KUWATUMIKIA WANANCHI
Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Jumanne Sagini (kulia), Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof.
Elisante Ole Gabriel wakiwa katika nyuso za furaha mara baada ya kumalizika kwa
mazungumzo baina yao ambayo awali yalitanguliwa na kutembelea jengo kuu
la Mahakama ya Tanzania Tambukareli jijini Dodoma, Julai 11, 2024.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akimwelezea Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Jumanne Sagini kuhusu utendaji kazi wa kituo cha huduma kwa mteja
cha Mahakama kilichopo Tambukareli jijini Dodoma, Julai 11, 2024.
Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Jumanne Sagini (Kulia), Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof.
Elisante Ole Gabriel wakiwa wamesimama mbele ya Ukumbi wa Mahakama
namba mbili, ambao utatumika kwa ajili ya kusikiliza kesi mbalimbali pindi
utakapomalizika. Julai 11, 2024 Dodoma.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Hyasinta
Kissima, WyKS Dodoma
Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Jumanne Sagini Julai 11, 2024 jijini Dodoma, amekutana na
kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel,
ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya kuzitembelea na kujifunza majukumu ya
Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.
Katika mazungumzo hayo
yaliyotanguliwa na kulitembelea jengo la Makao Makuu ya Mahakama yaliyopo
Tambukareli jijini Dodoma, Naibu Waziri amefurahishwa na maboresho
makubwa yaliyofanywa na Mhimili wa Mahakama ikiwemo ujenzi wa jengo
la Mahakama lenye Teknolojia na vifaa vya kisasa ambalo litakuwa miongoni
mwa majengo makubwa sita bora Duniani lenye thamani ya Shilingi Bilioni 129.7
fedha kutoka mapato ya ndani ya Serikali.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama
Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kuwa, maboresho yanayofanywa katika Mhimili
wa Mahakama kama vile upatikanaji wa vifaa vya kisasa, rasilimali watu, ujenzi
wa miundombinu ya kisasa, matumizi ya TEHAMA, yameleta mchango mkubwa katika
ubora wa utoaji haki Nchi na imani ya Wananchi kwa Mahakama imeongezeka
maradufu.
"Nilipopewa jukumu la
kumsaidia Mhe. Waziri Dkt. Balozi Pindi Chana katika Wizara ya Katiba na
Sheria, nilisema lazima nijue hiki ninachoenda kukifanya.Tunapokea ripoti
mbalimbali na tunazisoma. Lakini, ningeishia kwenye ripoti pekee bila
kufika katika jengo hili na nimetembelea jengo hili sura ni tofauti
kabisa.” Alisema Sagini.
Aliendelea kusema,
"Nimeona makubwa kwenye TEHAMA. Jaji Mkuu aliniambia uje utembelee kwa
kweli mna maajabu. Ninaweza kuona taarifa ya Mahakama ya Mkoa fulani,
inafanya nini, shauri gani limepangwa kusikilizwa, mashahidi au hukumu
inatolewa kwamba hiyo taarifa ninaweza kuipata hapa. Lakini malalamiko ya
Wananchi kituo cha huduma kwa mteja kwamba kutakuwa na watu masaa 24 kusikiliza
kero za Wananchi, na kuzitafutia masuluhisho, huu ni ubunifu mkubwa sana.
Niwapongeze Mahakama kwa dhati ya moyo wangu kuwa mmefanya ubunifu katika
kuwatumikia Wananchi."
Naibu Waziri Sagini
amemshukuru Rais wa wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuja na wazo
la ujenzi wa jengo la Mahakama 2012, kutambua jitihada za Hayati Dkt.
John Pombe Magufuli kwa kuanza ujenzi 2020 na Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan 2021 kuendeleza ujenzi kwa kasi na kukubali kotoa fedha zote mpaka
kufikia hatua hiyo.
Naibu Waziri Sagini amesema
kuwa, Wizara ya Katiba na Sheria inaimani na kazi kubwa inayofanywa na Mahakama
na itaendelea kushirikiana nao na kuisemea Mahakama katika majukwaa mbalimbali
na pia kuitumia Mahakama kupitia maboresho yaliyofanyika kuwa sehemu ya eneo la
kujifunza kwa Taasisi mbalimbali zilizopo chini ya Wizara na zinazohusika
katika utoaji wa Haki kwa Wananchi.
Comments
Post a Comment