SERIKALI YAELEZA JISI TANZANIA ILIVYOJIPANGA KUPAMBANA NA MATUKIO YA UKATILI KWA WATU WENYE UALBINO.
Waziri wa Katiba na Sheria
Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana pamoja na ujumbe wa Tanzania walipofanya
mazungumzo kwa njia ya mtandao na Mtaalam wa kujitegemea anayehusika na masuala
ya Haki za watu wenye ualbino Bi. Muluka-Anne Miti-Drummond, Julai 4, 2024
Geneva.
xxxxxxxxxxxxxx
Na
Lusajo Mwakabuku – WKS Geneva
Tanzania imekuwa ni nchi
inayotazamwa zaidi na mashirikia mbalimbali ya kimataifa yanayohusika na Haki
za Binadamu hususan Matukio ya ukatili kwa watu wenye ualbino ambayo yameendelea
kujitokeza mara kwa mara.
Hayo yameelezwa na Bi.
Muluka-Anne Miti-Drummond ambaye ni mtaalam wa kujitegemea anayehusika na
masuala ya Haki za watu wenye ualbino alipofanya mazungumzo kwa njia ya mtandao
(Zoom Meeting) na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Hazara
Chana leo tarehe 04/07/2024.
Akielezea suala hilo, Bi
Muluka-Anne amesema linapofika suala la ukatili wa watu wenye ualbino nchi ya
Tanzania imekuwa ikishika nafasi ya juu kuandikwa katika vyombo mbalimbali vya
Habari na hata mitandao ya kijamii, suala lililowafanya wao kuiangalia Tanzania
kwa jicho la kipekee yanapokuja masuala yanayohusu watu wenye ualbino nchini.
Bi. Muluka akasema suala
hilo limezua taharuki miongoni mwa wazazi ambao watato wao wana ualbino kiasi
wanashindwa hata kuwaacha waende shule wakihofia usalama wao na suala hili kwao
limekuwa changamoto kubwa wakati wakiandika ripoti kwani wanashindwa kushauri
jinsi ya kuwalinda watu wenye ualbino kwani kuwaweka katika sehemu maalumu ni
kuwanyima haki ya kuishi na familia zao.
Akijibu hoja hizo, Waziri wa
Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana alisema Tanzania inafanya
juhudi kubwa katika kuhamasiha jamii jinsi ya kuondokana na imani potofu ambayo
ndio inasemekana kuwa chanzo kikubwa cha ukatili huu kwa kupitia njia
mbalimbali zikiwemo vyombo vya Habari, mikutano ya hadhara na vyombo vya dini
kama Makanisa na Misikiti katika maeneo mbalimbali.
Aidha, Pindi Chana alieleza
kuwa Tanzania inasimamia ipasavyo sheria hususan zile zinazohusika na masuala
ya ubaguzi na kwamba hili suala limetengenezewa mkakati wa kitaifa na hivi
karibuni Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa akizungumza Bungeni
amesema hatua ya kuwalinda watu wenye ualbino ni jambo linalopaswa kutelelezwa
na makundi yote ya jamii na kwa upande wake Serikali imeweka hatua kadhaa
ambazo utekelezaji wake utahusisha wakuu wa mikoa, wilaya, vyombo vya dola,
viongozi wa dini pamoja na watoa tiba za jadi.
Pamoja na jitihada hizo,
Pindi chana alieleza kuwa Serikali inahakikisha upatikanaji wa vikingajua ikiwa
ni pamoja na kutoa kodi kwenye uingizaji wa dawa na vifaa ambavyo watu wenye
ualbino wanavipata.
Comments
Post a Comment