TANZANIA NI NCHI YA MFANO KWA KUPOKEA NA KUWAHIFADHI WAKIMBIZI.
Waziri wa Katiba na Sheria
Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana alipofanya mazungumzo na Kamishna Mkuu Msaidizi wa
shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Bw. Raouf Mazou, Julai
4, 2024 Geneva.
Waziri wa Katiba na Sheria
Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana na Kamishna Mkuu Msaidizi wa shirika la Umoja wa
Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Bw. Raouf Mazou, kwenye picha ya pamoja na
ujumbe wa Tanzania, Julai 4, 2024 Geneva.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na
Lusajo Mwakabuku – WKS GENEVA
Tanzania imetajwa kuwa nchi
ya mfano katika kuwapokea na kuwahifadhi wakimbizi toka enzi za Rais wa Awamu
ya Kwanza Hayati Julius Kambarage Nyerere.
Hayo yameelezwa na Kamishna
Mkuu Msaidizi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR bwana
Raouf Mazou, alipofanya mazungumzo na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi
Dkt. Pindi Hazara Chana tarehe 04/07/2024 Ofisini kwake yalipo Makao Makuu ya
Shirikika hilo Geneva, Switzerland.
Kamishna Mazou aliongeza
kuwa Tanzania ukilinganisha na nchi nyingine imekuwa ikipokea wakimbizi na
kuwapatia mahitaji muhimu na pia akatumia nafasi hiyo kugusia suala la elimu
kwamba watoto wanaoishi katika maeneo ya wakimbizi waweze kupatiwa elimu bora
na itakayoweza kuwasaidia kuendelea kimasomo mara wanaporudi nchini mwao.
Kwa upande wake Waziri Chana
alisema Serikali inaendelea na jitihada za kuongeza uhamasishaji katika maeneo
ambayo wanaingilia wakimbizi kama vile Kigoma kama ambavyo Mwalimu Nyerere
alisema kuwa tofauti ni mipaka ila waafrika ni wamoja na pia akatoa mfano wa
Rais Kabila ambaye anaye alikuwa mkimbizi nchini Tanzania na akaweza kurudi
nchini kwao na kuwa kiongozi.
Akijibu suala la elimu,
Waziri Chana alisema akirudi nchini atawasiliana na Waziri wa Mambo ya Ndani
pamoja na Waziri wa Elimu kuona ni namna gani wataweza kufanikisha hilo na pia
akatumia nafasi hiyo kumwomba Kamishna Mazou kuangalia nafasi zozote za
ushirikiano katika masuala ya uwezeshaji kwa watu wanaowashughulikia wakimbizi
nchini Tanzania.
Comments
Post a Comment