TUISHAURI SERIKALI TUSIKAE KIMYA - SAGINI
Naibu Waziri wa Katiba
na Sheria Mhe. Jumanne Sagini akizungumza na Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali (hawapo pichani) Julai 2, 2024 wakati alipowatembelea jijini
Dodoma kwa lengo la kujitambulisha na kufahamu majukumu yao.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Khatibu Kazungu akizungumza na Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (hawapo pichani) Julai 2, 2024 jijini Dodoma.
Kikao cha Menejimenti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Julai 2, 2024 jijini Dodoma.
Watumishi wa Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakimsikiliza Naibu Waziri wa Katiba na Sheria
Mhe. Jumanne Sagini alipowatembelea jijini Dodoma Julai 2, 2024.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Hyasinta
Kissima - WKS Dodoma
Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Jumanne Sagini ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
kwa kuendelea kusimamia jukumu lake la msingi la kuishauri Serikali
katika masuala yote ya Kisheria ndani na Nje ya Nchi ambapo ameelekeza Ofisi hiyo
kuendelea kusimamia haki, uadilifu na kuishauri Serikali kwa hekima na heshima.
Naibu Waziri Sagini
aliyasema hayo Julai 2, 2024 jijini Dodoma, wakati akizungumza katika
kikao na Menejimenti na Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mhe. Sagini amesema
kuwa katika uandaaji wa Sheria inapoonekana kunaweza kuibuka ukakasi
katika utekelezaji wake ni vyema Ofisi hiyo ikatoa taarifa mara moja kwa
Viongozi na kushauri ipasavyo ili kuzuia madhara kwa Serikali na
Wananchi.
"Ninyi ni Taasisi ya
Kikatiba. Tunaona jitihada kubwa zinazofanywa katika kuimarisha msaada wa
Kisheria ikiwa ni pamoja na kuendelea kusimamia nidhamu ya Mawakili wa
kujitegemea kwani wapo ambao wanawaonea Wananchi. Panapotokea jambo ambalo
mnaona Kisheria linaweza kuleta maneno ni vyema mkaliwasilisha na mkatumia
taaluma yenu kushauri badala ya kukaa kimya. Mnafanya kazi kubwa sana endeleeni
kutimiza wajibu wenu kwa maslahi makubwa ya Nchi yetu na pia endeleeni
kuimarisha umoja na mshikamano pahala pa kazi." Alisema Naibu Waziri
Sagini.
Kwa upande wake Naibu Katibu
Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Khatibu Kazungu amesema kuwa, Wizara kwa
sasa imeanza kuandaa maandiko ya miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa kuwajengea
uwezo Wanasheria ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na moja kati ya
mambo yaliyokusudiwa kupitia mradi huo ni kuimarisha utendaji kazi wa
Wanasheria katika maeneo mbalimbali yanayoibuka kwenye taaluma hiyo na ambayo
mara nyingi hayapatikani katika Vyuo hapa Nchini.
Awali akiwasilisha taarifa
ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hiyo kwa Naibu Waziri, Naibu Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Mhe. Prof. Kennedy Gastorn amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali kwa kipindi cha mwaka 2023/2024, imepata mafanikio kadha wa kadha
ikiwa ni katika kufanikisha Urekebu wa Sheria kuu 446 ili toleo la Sheria
lililofanyiwa urekebu kwa mwaka 2023 liweza kutoka, kufanya tafsiri ya Sheria
300, kuhakiki Sheria ndogo 1228, kufanya upekuzi kwa hati za makubaliano 34,
kutoa maoni 1707 kwenye Wizara na Taasisi na kufanikisha miswada 19
iliyoandaliwa ambapo miswada 17 ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kuwa Sheria.
Comments
Post a Comment