WAZIRI CHANA AONGOZA MAPOKEZI YA KATIBU MKUU KATIBA NA SHERIA

Bwana Eliakim Chacha Maswi akila kiapo kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Julai 26, 2024 Ikulu Dar es Salaam.


Bwana Eliakim Chacha Maswi (mwenye shada la maua) baada ya kupokelewa na Viongozi wa Wizara na baadhi ya Wakuu wa Taasisi za Wizara, Julai 26, 2024 Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Dar es Salaam.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana akiongea kwenye hafla ya kumkaribisha Katibu Mkuu Maswi, Julai 26, 2024 Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini akiongea kwenye hafla ya kumkaribisha Katibu Mkuu Maswi, Julai 26, 2024 Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Dar es
Salaam.

Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Eliakim Chacha Maswi akiongea na Viongozi wa Wizara na baadhi ya Wakuu wa Taasisi za Wizara kwenye hafla ya kumpokea kama Katibu Mkuu mpya, Julai 26, 2024 Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Khatibu Kazungu akielezea kwa kifupi majukumu ya Wizara kwenye hafla ya kumkaribisha Katibu Mkuu Maswi, Julai 26, 2024 Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Dar es Salaam.


Bwana Eliakim Chacha Maswi (wa pili kulia) kwenye picha ya pamoja na Viongozi wa Wizara na baadhi ya Wakuu wa Taasisi za Wizara baada ya kupokelewa, Julai 26, 2024 Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Dar es Salaam.


xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Na Lusajo Mwakabuku - WyKS Dar es salaam.

Waziri wa katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amewaongoza Viongozi wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo na watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kumpokea na kumpongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Eliakim Maswi kwa kuteuliwa na kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassani.

Akizungumza mara baada ya hafla ya uapisho uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Mhe Balozi Daktari Pindi Chana amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumteua Bw. Maswi kushika nafasi hiyo kwa kuwa ni mtu mwenye uzoefu na maarifa hivyo ataiwezesha Wizara ya Katiba na Sheria kuendelea kupiga hatua katika kuliletea taifa maendeleo.

Akizungumza wakati wa mapokezi hayo Mhe. Waziri Chana amemwelezea kiongozi huyo kama mtu mchapakazi na mwenye uzoefu wa muda mrefu katika utumishi wa umma kwa kuwa amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini huku akiahidi kumpa ushirikiano mkubwa ili kwa pamoja waweze kumsaidia Mhe. Rais wa Jamhuri ya Mkuungano wa Tanzania kuwaletea wananchi maendeleo.

Akimkaribisha Kiongozi huyo Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini amemkaribisha Mhe. Maswi kwenye familia ya Wizara ya Katiba na Sheria ili waendelee kushirikiana vyema kutekeleza majukumu ya Wizara ikiwa ni sehemu ya kuendeleza kazi kubwa iliyofanywa na mtangulizi wake Bi. Mary Makondo aliyeteuliwa na Mhe. Rais kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma.

Mhe. Sagini amemwelezea Mhe. Maswi kama mtu shupavu anayefanya kazi kwa bidii bila kuchoka usiku na mchana huku akiweka wazi kuwa anayo furaha kubwa kumpongeza kwa dhati Mhe. Maswi kwa kuteuliwa na kuapishwa kama Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria huku akibainisha kuwa kuteuliwa kwake ni ishara ya imani kubwa ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anayo kwake na uwezo wake wa kuleta mabadiliko chanya katika Wizara hii muhimu nchini.

“Nina imani kubwa kuwa uongozi wako utaimarisha utendaji wa Wizara na kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya sheria, tunaahidi kukupa ushirikiano.” Alisema Mhe. Sagini.

Akiongea mbele ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi amesema kuwa amefanya kazi na Mhe. Maswi wakati akiwa kiongozi katika nafasi mbalimbali na kueleza kuwa anatambua jitihada zake kama kiongozi anaependa kujitolea katika kuhakikisha utawala bora na uimarishaji wa sekta ya sheria na kusisitiza kuwa anaamini kuwa chini ya uongozi wake wananchi watashuhudia maboresho makubwa na mafanikio katika nyanja mbalimbali za sekta ya sheria nchini.

Naye Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende kando ya kumpongeza kiongozi huyo kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo muhimu, ametumia nafasi hiyo kumweleza kiongozi huyo majukumu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambayo ni kuendesha, kuratibu na kusimamia mashauri yote ya Madai, Usuluhishi, Katiba, Haki za Binadamu na Uchaguzi yanayofunguliwa na Serikali au dhidi ya Serikali ndani na nje ya nchi. Dkt. Luhende ameahidi kumpa ushirikiano kiongozi huyo na kumtakia kila la heri katika majukumu yake mapya huku akimwomba kuendelea na moyo wa kujituma kwa maendeleo ya taifa letu.

Akizungumza mara baada ya kukaribishwa na viongozi hao Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Eliakim Maswi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani kubwa aliyonayo kwake na kuamua kumteua katika nafasi hiyo huku akiomba viongozi hao kufanya kazi kwa bidii kwa kuwa wote wanafanya kazi ya kujenga nyumba moja.

Bw. Eliakim Maswi aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Tarehe 21 Julai, 2024. Kabla ya Uteuzi huo Bw. Maswi alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).





 

Comments

Popular posts from this blog

USAJILI WA VIZAZI NA VIFO NI TAKWA LA KISHERIA

UONGOZI WA MAHAKAMA YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU NA WATU YAKUTANA NA VIONGOZI WA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA

BODI YA KITAIFA YA USHAURI YA MSAADA WA KISHERIA YATEMBELEA WASAIDIZI WA KISHERIA IRINGA