WAZIRI CHANA NA BALOZI POSSI WAKUBALIANA KUIMARISHA UTENDAJI KAZI WA WATUMISHI

 

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akisalimiana na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Geneva Switzerland Mhe. Balozi Dkt. Abdallah Possi, Julai 01, 2024 Geneva Switzerland.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akishiriki kikao cha 56 cha Baraza la Haki za Binadamu kinachoendelea jijini Geneva – Switzerland, Julai 01, 2024.

Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo akiongea wakati ujumbe wa Waziri wa Katiba na Sheria ulipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Geneva Switzerland Mhe. Balozi Dkt. Abdallah Possi, Julai 01, 2024.

MKurugenzi Idara ya Haki za Binadamu Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Nkasori Sarakikya akiteta jambo na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Geneva Switzerland Mhe. Balozi Dkt. Abdallah Possi, Julai 01, 2024 Geneva Switzerland.

Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Geneva Switzerland Mhe. Balozi Dkt. Abdallah Possi, akiongea na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana na ujumbe alioambatana nao, Julai 01, 2024 Geneva Switzerland.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Na Lusajo Mwakabuku – WKS Geneva, Switzerland

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Geneva Switzerland Mhe. Balozi Dkt. Abdallah Possi ambapo Waziri Chana alitumia nafasi hiyo kumwomba Balozi Possi kuangalia fursa mbalimbali ambazo watumishi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria wanaweza kuzipata hapa Geneva.

Waziri Chana amezungumza hayo leo tarehe 01/07/2024 alipofika katika katika Ofisi ya Ubalozi jijini Geneva ikiwa ni sehemu ya ushiriki wa Mhe. Waziri na ujumbe wake katika kikao cha 56 cha Baraza la Haki za Binadamu kinachoendelea jijini Geneva - Switzerland.

Akizitaja fursa hizo, Waziri Pindi Chana alisema ushiriki wa wataalam wetu katika vikao na warsha mbalimbali ni muhimu lengo likiwa ni kuhakikisha nchi inapata uwakilishi wa kutosha katika maeneo mbalimbali na hivyo kutangaza vizuri nchi yetu katika anga za kimataifa lakini pia watumishi wakiongeza uelewa katika utendaji kwa kubadilishana uzoefu na watumishi kutoka mataifa mengine.

Aidha, Waziri Pindi Chana akaongeza kuwa kutokana na maendeleo ya kiteknolojia Balozi anaweza watafutia nafasi za kushiriki warsha kwa njia ya mtandao (Zoom n.k) ambavyo si lazima mshiriki kuwepo eneo ambalo mkutano unafanyikia.

Akizungumza baada ya maelezo ya Waziri, Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo amesema Wizara kwa upande wa Tanzania Bara kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea na jitihada mbalimbali katika  kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinaendelea kuimarishwa nchini Tanzania. Aidha, akasisitiza kwa upande Ubalozi kuweza kutafuta nafasi mbalimbali zikiwemo internship kwa lengo la kuongeza uwezo wa kufikiri kwa wataalam baada ya kupata uzoefu kutoka mataifa mengine.

Akiongelea kuhusu suala la kujengea uwezo watumishi, Balozi Possi alikubali kuwa suala hilo ni mtambuka na lina tija hivyo akaomba yaainishwe mahitaji kwa maandishi katika maeneo ambayo Wizara ingependa wataalam wajengewe uwezo ili yeye na Ofisi yake aweze kuwasiliana na Wadau na kuona jinsi ya kuliwezesha hilo huku akikiri kuwa suala hilo linatekelezeka.

Kikao cha 56 cha Baraza la Haki za Binadamu kinaendelea leo jijini Geneva- Switzerland katika ofisi za Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa ambapo leo mada iliyojadiliwa ni kuhusu utunzaji wa mazingira na masuala ya mabadiliko ya tabianchi.






Comments

Popular posts from this blog

USAJILI WA VIZAZI NA VIFO NI TAKWA LA KISHERIA

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA