WIZARA YA YASHIRIKI KATIKA UZINDUZI WA MAONESHO YA KIBIASHARA YA SABASABA
Hyasinta
Kissima – WKS Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Jumanne Sagini Julai 3, 2024 ameiwakilisha Wizara katika uzinduzi
wa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba yaliyofunguliwa rasmi
na Rais wa Msumbiji, Mhe. Filipe Jacinto Nyusi akiambatana na mwenyeji
wake Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika uzinduzi
wa Maonesho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema
kuwa kampuni zaidi ya 11 Nchini zimeanza kunufaika na ufanyaji wa biashara
katika Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA).
"Serikali itaendelea
kutatua changamoto za Wafanyabiashara na katika Wizara milango ipo wazi kwa
ajili ya kuwasikiliza." Alisema
Rais Samia.
Katika hatua nyingine Waziri
wa Wizara ya Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb)
aliongozana na Mhe. Sagini, Mhe. Chiwelesa pamoja na viongozi wengine
kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii.
Katika kutembelea banda la
Wizara ya Maliasili na Utalii, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne
Sagini (Mb), ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ubunifu wa kuyaalika
makabila mbalimbali likiwemo kabila la Wazanaki lililopo katika
wilaya ya Butiama mkoani Mara.
"Jambo lililonifurahisha
zaidi ni kukutana na kabila la Wazanaki katika maonesho haya ya Kimataifa
ya kibiashara. Kupitia tamaduni hizi tunazozioana hapa za Wazanaki
ikiwemo kusaga kwa kutumia jiwe, vitanda na nyumba zilizokuwa zikitumika
zinatukumbusha tulipotoka na kuona mambo ambayo walikuwa wanayafanya Wazee
wetu. Niwaombe watu wafike kujifunza mema ya kabila la Wazanaki katika banda la
Wizara ya Maliasili na Utalii." Alisema Sagini.
Ikumbukwe kuwa katika Maonesho
hayo, Wananchi mbalimbali kutoka nje na ndani ya Nchi hupata fursa ya
kuonesha shughuli zao jambo ambalo husaidia kukuza uchumi, ajira na
kuongeza mapato ya Serikali.
Comments
Post a Comment