WOTE TUNA HAKI SAWA TUWAJALI WENYE MAHITAJI MAALUM – MAKONDO
Baadhi ya wajumbe na washiriki
wa uzinduzi wa Mradi wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia Mbadala kwa watu wenye
ulemavu, Julai 12, 2024 Jijini Dar es salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo akizindua rasmi Mradi wa Utatuzi wa Migogoro
kwa Njia Mbadala kwa watu wenye ulemavu, Julai 12, 2024 Dar es Salaam.
Erick Mukiza, Mkurugenzi
Mtendaji wa ESS Creative & Legal Foundation (ESS) akielezea malengo ya
kuanzisha Mradi wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia Mbadala kwa watu wenye ulemavu,
Julai 12, 2024 Dar es Salaam.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na Lusajo Mwakabuku – WyKS Dar es salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba
na Sheria Bi. Mary Makondo amewataka Watanzania kwa ujumla kuwajali na kuwapa
huduma zinazostahili watu wenye ulemavu kwani nao wana haki sawa katika jamii
pamoja na kwamba ni kundi linalosahaulika katika masuala mbalimbali ya kijamii.
Bi. Makondo ameyasema hayo leo
tarehe 12/07/2024 katika ukumbi wa American Corner uliopo Makumbusho ya Taifa
Jijini Dar es salaam akimwakilisha Waziri wa Katiba na Sheria kama Mgeni Rasmi
katika Hafla ya Uzinduzi wa Mradi wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia Mbadala kwa
watu wenye ulemavu.
Akisoma hotuba yake katika
hafla hiyo, Bi. Makondo alisema sisi wote ni watu wenye mahitaji maalum
watarajiwa sababu huwezi kujua kesho kitakupata kitu gani ndio maana ukiwaona
hawa ujue wewe ni sehemu yao na kusisitiza kuwa ni lazima tuwahudumie kwa
upendo na maadili.
“Matarajio ya Wizara ya Katiba
na Sheria na Serikali kwa ujumla katika kushiriki kwenu katika mradi huu ni
pamoja na kuwa kichocheo katika kusimamia na kutatua migogoro na kupunguza
idadi ya kesi kupitia upatanishi hivyo kuimarisha juhudi za Serikali kupunguza
mrundikano wa kesi Mahakamani, na
kushauri Serikali na taasisi zake wakiwemo viongozi katika ngazi
mbalimbali za kushughulikia na kutatua migogoro kwa watu wenye ulemavu.”
Alisema Bi. Makondo.
Makondo ametoa rai kwa
wahusika kuhakikisha wanafuata kanuni za maadili za upatanisho wa migogoro kwa
kuwa na tabia na mwenendo unaohakikisha haki, uadilifu, usiri, uwajibikaji na
usawa.
“Tumesikia wakati dada akitoa
shuhuda pale alisema kwamba anawashukuru wanasheria kwa kuendelea kuwa
waadilifu kwa hiyo tuendelee kuwa waadilifu na kujali wengine na kuzingatia
kwamba ulinzi wa haki ya mtu mwingine ni jukumu lako,” aliongeza.
Akielezea mradi huo, Erick
Mukiza, Mkurugenzi Mtendaji wa ESS Creative & Legal Foundation (ESS)
amesema lengo la kuanzisha mradi huo limetokana na tafiti mbalimbali katika
bara la Afrika ambazo zimeonesha kuwa utatuzi wa migogoro bila kwenda
Mahakamani imewasaidia wanawake wengi
kuweza kupata haki zao, lakini kwa upande wa Tanzania, watu wenye
ulemavu hususan wenye ulemavu wa kusikia wameachwa nyuma hasa katika suala la
kupata taarifa na faida za Utatuzi wa Migogoro kwa Njia Mbadala.
“Utatuzi wa Migogoro kwa Njia
Mbadala (Altenative Disputes Resolutions - ADR) umeonekana kuwa njia bora zaidi
na ya gharama nafuu katika kutatua migogoro nje ya shauri la Mahakama ikiwa ni
pamoja na kuilinda amani kupitia upatanisho unaopatikana nje ya vifungu vya
kisheria kama ambavyo Jaji Mkuu na Rais wa Tanzania wameelezea katika matukio
tofauti tofauti.” Alisema Bwana Mukiza.
Awali akitoa salamu za
ukaribisho kwa Mgeni Rasmi, Mwenyekiti wa Board ya ESS Creative & Legal
Foundation (ESS) Dkt. Elly Ndyetabula alisema, “kutatua migogoro kwa njia
mbadala inaokoa muda lakini pia inaendeleza mahusiano, tunakuwa na urafiki kwa
sababu migogoro inatatuliwa kwa maridhiano.”
Comments
Post a Comment