PINDI CHANA AFANYA ZIARA YA UKAGUZI WA USAJILI WA WATOTO DODOMA
Na
Lusajo Mwakabuku - WyKS Dodoma
Waziri wa Katiba na Sheria
Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana leo Agosti 09, 2024 amefanya ziara na kukagua
zoezi la usajili na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto wa umri chini ya miaka
mitano katika hospitali ya St. Gemma, Kituo cha afya Makole na Zahanati ya Kikuyu Jijini Dodoma.
Katika ziara hiyo Waziri
Chana, amewataka wananchi kuhakikisha watoto wao wanasajiliwa na kupatiwa vyeti
vya kuzaliwa mara baada ya kujifungua kabla ya kuruhusiwa kurudi nyumbani.
"Ndugu Wananchi hasa kina
mama wenzangu, Serikali yetu inayoongozwa na Mhe. Rais Mama Samia Suluhu Hassan
imewaletea huduma hii ya vyeti vya kuzaliwa bure kwa watoto wetu hivyo hii ni
fursa kwenu kwani vyeti hivyo vitawasaidia kupata huduma ya matibabu kupitia
bima ya afya, baadaye elimu na ajira." Alisema.
Pia Waziri Mhe. Balozi Dkt.
Pindi Chana aliwakabidhi vyeti vya kuzaliwa baadhi ya akina mama waliojifungua
salama na kuruhusiwa katika vituo hivyo vya tiba.
Akizungumza kwa niaba ya
Wanawake waliokuwa wakipatiwa huduma
hiyo Bi. Halima Abdallah ameishukuru Serikali kwa kuwasogezea huduma hiyo na
kuahidi kuwa balozi kwa kuwaelimisha ndugu, marafiki na majirani kuhusu upatikanaji
wa huduma hiyo na umuhimu wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto.
Comments
Post a Comment