SERIKALI INARIDHISHWA NA KAZI ZA WASULUHISHI
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne
Abdallah Sagini akisoma hotuba kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Prof. Palamagamba Kabudi katika Mkutano wa Mwaka wa Taasisi ya Wasuluhishi
Tanzania (Tiarb) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hotel ya Protea
Malliot jijini Dar es salaam, tarehe 23/08/2024.
Rais wa Taasisi ya Usuluhishi Tanzania (TIArb),
Madeline Kimei akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri wa
Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Abdallah Sagini aliyemwakilisha Waziri wa Katiba
na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi katika Mkutano wa Mwaka wa Saba wa Taasisi ya Wasuluhishi Tanzania (Tiarb),
23/08/2024.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne
Abdallah Sagini akiwa meza kuu katika Mkutano wa Mwaka wa Taasisi ya
Wasuluhishi Tanzania (Tiarb) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hotel ya
Protea Malliot jijini Dar es salaam tarehe 23/08/2024.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne
Abdallah Sagini akifuatilia matukio katika Mkutano wa Mwaka wa Taasisi ya
Wasuluhishi Tanzania (Tiarb) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hotel ya
Protea Malliot jijini Dar es salaam, tarehe 23/08/2024.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Abdallah Sagini na viongozi wa Tiarb na baadhi ya wanachama wakiwa katika picha ya pamoja, tarehe 23/08/2024
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na
Lusajo Mwakabuku - WyKS Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Jumanne Abdallah Sagini amesema Serikali inaridhishwa na juhudi
zinazofanya na taasisi mbalimbali zinazoshughulikia masuala ya upatanishi
kwenye migogoro mbalimbali hususan migogoro ya biashara.
Mhe. Sagini ameyasema hayo tarehe
23/08/2024 alipokuwa akimwakilisha Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof.
Palamagamba Kabudi katika Mkutano wa Mwaka wa Taasisi ya Wasuluhishi Tanzania
(Tiarb) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hotel ya Protea Malliot jijini
Dar es salaam.
Akiwasilisha salamu za Waziri
Kabudi, Mhe. Sagini alisema migogoro inayomalizika nje ya Mahakama inatumia
muda mfupi kuliko ile inayofuata taratibu za
kimahakama ambayo mara nyingi upande mmoja hasa ule ulioshindwa unabaki na maumivu yanayopelekea kujengeka
kwa uhasama baina ya pande hizo mbili.
“Tukiweza kuweka juhudi za
pamoja katika kuimarisha matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro
tutaweza kufanikisha malengo ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
(1977) ya kutochelewesha haki bila sababu ya kimsingi [Ibara ya 107A (2) (b)];
kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya wanaohusika katika migogoro [Ibara ya
107A (2) (d)]; na kutenda haki bila kufungwa kupita kiasi na masharti ya
kiufundi yanayoweza kukwamisha haki kutendeka [Ibara ya 107A (2) (e)]” alisema
Mhe. Sagini.
Akizitaja faida hizo, Mhe.
Sagini alisema matumizi ya njia hizi mbadala huharakisha upatikanaji wa haki
kwa haraka na kwa watu wote, huokoa muda na gharama za wadaawa ambazo zinaweza
kutumika katika uzalishaji wa uchumi. Pia njia hizi mbadala zina faida nyingine
kubwa kama vile ushiriki wa wenye mgogoro katika kutafufa suluhu wao wenyewe,
kuwepo kwa usiri na faragha kwa wadaawa, kutumia njia zisizo na utaratibu mgumu
ambazo hukubalika kwa pande zote mbili pamoja na kuhifadhi mahusiano baina ya
wadaawa.
Aidha Mhe. Sagini aliongeza
kuwa Matumizi ya Usuluhishi yanafaida kubwa ya kupandisha hadhi na nafasi ya
Tanzania katika ripoti ya hali ya uwekezaji urahisi wa kufanya biashara
inayoweka viwango vya kimataifa katika upimaji wa mfumo wa ushughulikiaji wa
migogoro ya madai.
“Sote tutambue usuluhishi ni
dhana yenye kututaka tubadili fikra zetu za utoaji haki zilizojengwa na mfumo
wa utoaji haki unaochukua muda mrefu kabla ya mgogoro kumalizika kwa kufuata
ngazi za kimahakama kuanzia Mahakama za Mwanzo hadi ya Rufani, na kupitia katika
hatua nyingi, maahirisho mengi na mapingamizi mengi ya kiufundi ndani ya kila
ngazi za Mahakama”. Alihitimisha Mhe. Sagini.
Comments
Post a Comment