KATIBA NA SHERIA NA UONGOZI WA TLS WAKUBALIANA KUSHIRIKIANA

 

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akiongea katika kikao na Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili wa Tanzania (TLS) Mtumba Dodoma katika Ofisi za Wizara ya Katiba na Sheria 17/09/2024.

Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Eliakim Maswi akiongoza majadiliano ya wataalam baina na Menejimenti ya Wizara na Uongozi wa TLS kabla ya kumkaribisha Waziri wa Katiba na Sheria. 17/09/2024.

Rais wa TLS Bw. Boniface Mwabukusi akielezea kufurahishwa kwake na mapokezi tangu walipowasili Wizara ya Katiba kabla ya kuanza kuelezea hoja za ushirikiano. 17/09/2024.

Baadhi ya viongozi kutoka Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili wa Tanzania (TLS) wakifuatilia majadiliano katika kikao hicho. 17/09/2024.


Menejimenti ya Wizara na Uongozi wa TLS waliohudhuria katika kikao hicho wakifuatilia majadiliano. 17/09/2024.

Waziri wa Katiba na Sheria, Menejimenti ya Wizara na Uongozi wa TLS wakiwa katika picha ya pamoja. 17/09/2024.


xxxxxxxxxxxxxxxxx

Na Lusajo Mwakabuku & Hyasinta Kissima – WyKS Dodoma

Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili wa Tanzania (TLS) likiongozwa na Rais wa Chama hicho Bw. Boniface Mwabukusi wamekubaliana kwa pamoja na Wizara ya Katiba na Sheria chini ya Waziri mwenye dhamana Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu yote yanayohusu sekta ya sheria kwa kuzingatia mipaka na taratibu kwa maslahi mapana ya Taifa.

Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya kikao cha majadiliano kilichofanyika kwa zaidi ya saa sita katika ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Wizara yaliyopo Mtumba Jijini Dodoma tarehe 17/09/2024 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka TLS huku Wizara ya Katiba na Sheria ikiwakilishwa na Waziri wa Katiba na Sheria na Menejiment yote ya Wizara.

Katika kikao hicho hoja mbalimbali ziliibuliwa na kutokana na uzito wa majadiliano hayo, Waziri Kabudi alielekeza Baraza hilo la TLS likae kwanza na Menejimenti ya Wizara ikiongozwa na Katibu Mkuu bwana Eliakim Maswi kwa lengo la kujadili masuala ya kitaalamu na baada ya hapo ikafuatia awamu ya pili iliyomjumuisha Waziri.

Hoja mbalimbali ziliibuliwa katika kikao hicho moja wapo ikiwemo utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign – MSLAC) ambapo TLS waliitaka Wizara iwahusishe wanachama wengi zaidi wa TLS waliopo katika maeneo mbalimbali nchini lengo likiwa ni kuwa na mwendelezo wa huduma mara kampeni inapomalizika eneo husika. Waziri Kabudi alikubali ombi hilo na kuagiza iundwe Kamati ya pamoja itakayojumuisha wanachama wa TLS na kuangalia namna bora zaidi ya kuboresha utekelezaji wa kampeni hiyo.

Aidha jambo la pili lililojadiliwa ni pamoja na uanzishwaji wa Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi (Arbitration Center) ambachokitakuwa chombo cha kimataifa ambacho kitaweza kuhudumia watu wa nchini na kutoka mataifa mbalimbali. Na hili pia Waziri akaelekeza iundwe kamati na uandaliwe mpango mzuri juu ya uanzishwaji wa kituo hiki.

Katika hatua nyingine, Rais wa Chama hicho Bw. Mwabukusi akaiomba Wizara kupitia Taasisi zake hasa Tume ya Kurekebisha Sheria kuhakikisha kuwa TLS inashirikishwa katika kutoa maoni katika miswada mbalimbali kabla ya kufanywa kuwa sheria lengo ni katika kuhakikisha kunakuwa na sheria bora zaidi za kusaidia wananchi. Jambo ambalo Waziri Kabudi, kama ambavyo alikubali hoja zingine na hiyo aliikubali.

Akiongea mara baada ya kukamilika kwa kikao hicho, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi alisema anaamini kuwa huu ni mwanzo mzuri kwani wamekuwa na kikao kizuri chenye majadiliano marefu ya staha ambapo mambo mengi mazuri yenye kustawisha demokrasia ya nchi na ustawi wa jamii kupitia sekta ya sheria yamejadiliwa na kupatiwa ufumbuzi.

Kwa upande wake Rais wa TLS Bw. Mwabukusi alisema amefarijika kwa kiasi kikubwa kwanza kwa mapokezi ya heshima waliyopewa tangu Wizarani hapo na namna mjadala ulivyoendeshwa huku akisema huu ni mwanzo mzuri na wanatumaini kwa kusikilizana huku basi masuala mbalimbali yanayowahusu wananchi kisheria yatapatiwa ufumbuzi.

Hii ilikuwa ni ziara ya kwanza ya Rais wa TLS Bw. Mwabukusi kufika Wizarani kwa lengo la kujitambulisha tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo mwezi uliopita lakini kuwasilisha hoja mbalimbali za kiutendaji ambazo anadhani ni muhimu TLS na Wizara wakashirikiana.



Comments

Popular posts from this blog

USAJILI WA VIZAZI NA VIFO NI TAKWA LA KISHERIA

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA