MOCLA YAZINDUA KITUO CHA HUDUMA KWA MTEJA

 

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akihutubia katika hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja, Septemba 05, 2024 Mtumba Jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara Katiba na Ufuatiliaji Haki Bi. Jane Lyimo akitoa neno la utangulizi kwa niaba ya Katibu Mkuu Bw. Eliakim Maswi katika hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja, Septemba 05, 2024 Mtumba Jijini Dodoma.


Mkurugenzi Kitengo cha Uangalizi wa Utajiri wa Asili na Maliasili za Nchi DCP Neema Mwanga akitoa neno la ukaribisho kwa Wageni waliofika kwenye hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja, Septemba, 2024 Mtumba Jijini Dodoma.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja, Septemba, 2024 Mtumba Jijini Dodoma.


Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akimsikiliza na kumhudumia mwananchi kutokea Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora aliyepiga simu katika Kituo cha Huduma kwa Mteja akiuliza kuhusu usimamizi wa mirathi, Septemba 05, 2024 Mtumba Jijini Dodoma.

Mkurugenzi Idara ya Haki za Binadamu Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Nkasori Sarakikya akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Franklin Rwezimula mara baada ya kuzinduliwa rasmi kwa Kituo cha Huduma kwa Mteja, Septemba 05, 2024 Mtumba Jijini Dodoma.

Baadhi ya Wakurugenzi kutoka Idara mbalimbali chini ya Wizara ya Katiba na Sheria wakifuatilia hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja, Septemba 05, 2024 Mtumba Jijini Dodoma.


Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria na Wageni waalikwa walioshiriki uzinduzi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja, Septemba 05, 2024 Mtumba Jijini Dodoma.


xxxxxxxxxxxxxxxxx

Hyasinta Kissima – WyKS Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria  Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amesema Wizara yake imepanua wigo wa kuhudumia wananchi bila kuwalazimu kufika ofisi za Wizara kupitia Kituo cha Huduma  kwa Mteja.

Hafla ya kuzindua rasmi kituo hicho imefanyika tarehe 05 Septemba, 2024 Ofisi za Wizara Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma ambapo yeye alikuwa Mgeni Rasmi.

“Kupitia namba ya simu 026 216 0360 mwananchi anaweza kuwasilisha lalamiko lake na lalamiko hilo kufanyiwa kazi kwa wakati na kwa ufanisi bila mwananchi kulazimika kufika ofisi za Wizara. Huduma hii inasaidia kuwafikia wananchi wengi hususan wasio na uwezo wa kumudu gharama za usafiri kuja kuwasilisha malalamiko yao wizarani.” Alisema.

Wizara imeanzisha kituo hicho kupitia Programu ya Kujenga Uwezo wa Taasisi katika Kupambana na Rushwa (Building Sustainable Anti-Corruption Action in Tanzania – BSAAT) ili kupokea taarifa na malalamiko yanayohusu tuhuma za rushwa, ukiukwaji wa haki unaofanywa na taasisi ama mtu mmoja mmoja na maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi kuhusiana na huduma zinazotolewa na Wizara pamoja na Taasisi zote zilizo katika mnyororo wa utoaji haki.

Kituo hicho kimeanza kufanya kazi mwezi Februari, 2024 na hadi kufikia tarehe 31 Agosti, 2024 jumla ya malalamiko 499 yamesajiliwa, kati ya hayo malalamiko 410 sawa na asilimia 82 yamefanyiwa kazi kwa ukamilifu na 89 sawa na asilimia 18 yako katika hatua mbalimbali ya utekelezaji wake. Kwa sasa Kituo kinafanya kazi masaa yote ya kazi ila upo mpango wa kuongeza muda wa  kutoa huduma kituoni hadi masaa 24 katika siku saba za wiki.

Mafanikio yaliyopatikana baada ya kuanzishwa kwa kituo hicho ni pamoja na  kupokea malalamiko yanayohusu masuala ya kisheria; Kuratibu upatikanaji wa huduma za kisheria kwa wasiomudu gharama za wanasheria; Kupokea maoni, mapendekezo na ushauri juu ya huduma mbalimbali zinazotolewa na Wizara; Kupata mrejesho wa namna malalamiko yaliyoshughulikiwa na taasisi mbalimbali; Kuwarahisishia wananchi kufuatilia utekelezaji wa malalamiko yao kwa wakati pasipo kulazimika kufuata huduma hizo wizarani, hivyo kupata nafasi yakufanya shughuli za maendeleo.

Awali akitoa neno la utangulizi kwa niaba ya Katibu Mkuu Bw. Eliakim Maswi, Mkurugenzi wa Idara Katiba na Ufuatiliaji Haki Bi. Jane Lyimo amesema Kituo hicho kimeanzishwa baada ya Wizara kubaini kuwa malalamiko mengi ya wananchi yamekuwa yakiwasilishwa wizarani kwa njia ya barua au wananchi hao kufika moja kwa moja kwenye ofisi za Wizara kwa kutumia gharama kubwa za usafiri na kujikimu.  Vilevile, uwepo wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ambayo inaendeshwa na Wizara katika maeneo mbalimbali nchini imeibua uwepo wa malalamiko na hoja mbalimbali za kisheria kwa wananchi ambazo zinahitaji ufumbuzi wa haraka.


Comments

Popular posts from this blog

USAJILI WA VIZAZI NA VIFO NI TAKWA LA KISHERIA

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA