SAGINI AIPONGEZA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA NA KUITAKA KUZIJENGEA UWEZO KAMATI ZA MAADILI
Naibu Waziri wa Katiba
na Sheria Mhe. Jumanne Sagini (Mb), ameipongeza Tume ya Utumishi wa Mahakama
kwa kuendelea kusimamia kwa weledi ajira na nidhamu za Watumishi wa Mahakama
jambo ambalo limeongeza imani kubwa kwa Wananchi kwa Mahakama katika kusimamia
utoaji Haki Nchini.
Naibu Waziri Sagini ameyasema
hayo Septemba 23, 2024 jijini Dar es Salaam kwenye kikao na Watumishi wa
Tume hiyo ambapo Watumishi hao wameongozwa na Katibu wa Tume Prof.
Elisante Ole Gabriel na Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi
wa Mahakama Bi. Alesia Mbuya.
Mhe. Sagini amesema kuwa licha
ya kuwepo kwa kazi kubwa inayofanywa na Tume zipo Kamati za Maadili ya Maafisa
Mahakama katika ngazi ya Mikoa na Wilaya lakini Kamati hizo zimekuwa hazikutani
kujadili majukumu ya msingi licha ya kuwa vikao hivyo vipo kwa mujibu wa
Sheria.
"Kumekuwa na changamoto
ya uelewa na Bajeti kwa Kamati hizi kushindwa kutekeleza majukumu yao. Ni vyema
katika maandalizi ya bajeti tuone ni kwa namna gani Wizara zinaweza kuwasiliana
na bajeti hizo zikahusishwa katika mwongozo wa bajeti kwa ajili ya kuzihudumia
Kamati hizi." Alisema.
"Nitoe pongezi kwa Tume
kwa kuendelea kuzitembelea na kuzijengea uwezo Kamati hizi za Mikoa na Wilaya
ili ziweze kutambua majukumu waliyonayo na pia tuendelee kutoa elimu kwa jamii
kuhusu uwepo wa Kamati hizi ili waweze kutambua umuhimu na majukumu ya Kamati
katika kusimamia mnyororo wa Haki." Alisema Sagini.
Aidha, Naibu Waziri amesema
Serikali ya Awamu ya sita imeendelea kuonesha dhamira ya dhati na umuhimu wa
Tume hiyo ambapo kwa kipindi cha miaka minne kuongeza bajeti kutoka Bilioni 2.6
mpaka kufikia bilioni 5.5 mwaka 2024 ambapo inaonesha dhamira ya dhati ya Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuiwezesha
Tume katika kutekeleza majukumu yake.
Awali Katibu wa Tume ya
Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kuwa kwa sasa
Tume imejipanga kuendeleza matumizi ya mifumo katika masuala ya nidhamu
na maadili, lengo ikiwa ni kuhakikisha Kamati za Maadili za Wilaya na
Mikoa ziweze kutumia mifumo kujaza taarifa mbalimbali na kutunza
kumbukumbu ili kupunguza muda na gharama za Naibu Katibu wa Maadili
kufanya ufuatiliaji.
Comments
Post a Comment