VIONGOZI WA DINI MNA DHIMA KUBWA KATIKA KUHAKIKISHA AMANI NA UPENDO NCHINI – KABUDI
Waziri wa Katiba na Sheria
Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akiwa ameambatana na Shekhe Khawanja Muzaffar
Ahmad Amir na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahamadiyya Tanzania na
viongozi wengine wa dini ya kiislam wakiingia katika êneo la ukumbi
ulipofanyikia Mkutano Mkuu wa 53 wa Jumuiya ya Waislam Waahmadiyya, 27 Septemba, 2024 Dar es Salaam.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na
Lusajo Mwakabuku - WyKS Dar es Salaam.
Waziri wa Katiba na Sheria
Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi amesema viongozi wa dini nchini wana wajibu
mkubwa wa kuhakikisha upendo na amani vinatawala nchini kwa kupitia mafundisho
yao huku akiwasisitiza viongozi hao kuhubiri maadili ambayo hivi sasa yanaporomoka
kwa visingizio vya utandawazi na haki za binadamu.
Waziri Kabudi ameyasema hayo
tarehe 27/09/2024 alipoalikwa kama Mgeni Rasmi katika Mkutano Mkuu wa 53 wa
Jumuiya ya Waislam Waahmadiyya
uliofanyika katika eneo la Kitongoji cha Kitonga, kata ya Msongola
iliyopo wilaya ya Ilala jijini Dar es salaam.
Waziri Kabudi alianza kwa
kutoa shukrani kwa mwenyeji wake Shekhe Khawanja Muzaffar Ahmad Amir na
Mbashiri Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahamadiyya Tanzania kwa kumualika na
kuimwagia sifa taasisi ya kidini ya
Jumuiya ya Waislam Waahmadiyya Tanzania kuwa ni taasisi kongwe iliyofanya kazi
kubwa za kidini toka ilivyosajiliwa mwaka 1934, (Takriban Miaka 90) ambapo moja
wapo ya kazi hizo ni kutangaza uislam na kurahisisha waumini kuwa na uelewa wa dini
wanayoiamini kwani ni Jumuiya ya Kwanza kuandika Quran tukufu katika lugha ya
kiswahili.
Aidha Kabudi aliendelea kwa
kuwaomba viongozi wa dini waliohudhuria Mkutano huo wakiwemo, Mashekhe, Makhalifa
na Masharifu kuendelea kuhimiza upendo, mshikamano na kuheshimiana kama Taifa.
“Lazima tujue viongozi wa dini
mnayo dhima kubwa kuhakikisha amani na upendo katika Taifa letu, vinakuwa kipaumbele namba moja na
hayo yote yanawezekana ikiwa watu wetu watazingatia maelekezo ya dini zetu hasa
katika kuwatii viongozi wetu na kujua kuwa Mungu atawapokea wale wanaoamini na
kigezo muhimu cha wewe kuwa miongoni mwa wenye kuamini ni kuwa na upendo”.
Alisema Waziri Kabudi.
Akiongelea suala la utii na
maadili, Kabudi alisema “Upendo utatujengea utii na heshima baina yetu lakini
kwa Mwenyezi Mungu ameagiza tutii Mitume, Viongozi wetu na mkubwa kumheshimu
mdogo na mdogo kumheshimu mkubwa. Wakati huu tunapoelekea katika Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa niwasihi muwakumbushe waumini wenu kuongeza upendo na
kuwaheshimu na kuwatii viongozi wetu wa ngazi zote. Tukifanya hivyo tutakuwa
tunatimiza maamrisho ya Mwenyezi Mungu (Azza wa Jall) kwetu”.
Pia Kabudi akatumia nafasi
hiyo kuwaomba viongozi wa dini na watu wote wenye nafasi za kupaza sauti
kuendelea kuhimiza watu kushiriki uchaguzi ili kupata viongozi watakaotuongoza
katika kipindi cha miaka mitano ijayo huku akiwataka watanzania kujitokeza
kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la wapiga kura, na kujiandaa
kushiriki kikamilifu katika uchaguzi unaokuja wa Serikali za Mitaa.
Kabudi alihitimisha hotuba
yake kwa kuwahakikishia watu waliojitokeza katika mkutano huo kuwa milango ya
Wizara yake ipo wazi wakati wote na kuwakaribisha kwa masuala yoyote yanayohusu
sheria na upatikanaji wa haki huku akiongeza kuwa hivi karibuni alizindua Kituo
cha kisasa cha kupokea malalamiko yoyote yanayohusu rushwa kubwa na ndogo na
suala lolote linalopelekea uvunjifu wa haki nchini kwa kupiga simu kupitia namba 0262 160360.
Pia alimshukuru Mheshimiwa Dkt.
Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia
uanzishwaji wa Mama Samia Legal Aid Campaign, ikiwa ni utekelezaji wa sheria ya
Msaada wa kisheria sura 21, lengo likiwa ni kuwasaidia watanzania wote
wanaohitaji huduma za kisheria ila wanashindwa kuzifikia kwa sababu aidha, ya
kipato au sababu nyinginezo na kwamba
huduma hizi ni bure kabisa.
Comments
Post a Comment