BODI YA KITAIFA YA USHAURI YA MSAADA WA KISHERIA YATEMBELEA WASAIDIZI WA KISHERIA IRINGA
Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa
ya Ushauri ya Msaada wa Kisheria Bwana Saulo Malauri akifafanua jambo ikiwa ni
sehemu ya ziara ya bodi hiyo kutembelea mashirika wa wasaidizi wa
kisheria Mkoani Iringa, 24/10/2024.
Mratibu wa Shirika la Kilolo
Paralegal Unit akitoa Maelezo ya
utekelezaji kwa Bodi ya Kitaifa ya Ushauri ya Msaada wa Kisheria ilipofika
katika ofisi za shirika zilizopo Ilula wilayanii Kilolo tarehe 24/10/2024.
Wajumbe wa Bodi na wasaidizi
wa kisheria wa Kilolo Paralega Unit wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya
kumaliza mazungumzo patika shirika hilo. Tarehe 24/10/2024.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na
Lusajo Mwakabuku – WyKS Iringa
Bodi ya Kitaifa ya Ushauri ya
Msaada wa Kisheria ikiwa katika kikao kazi cha Kumi kinachofanyika kwa siku
mbili Mkoani Iringa imefanya ziara ya kuwatembelea watoa huduma za msaada wa
kisheria waliopo Iringa Mjini na Wilaya ya Kilolo kwa lengo la kukagua utekelezaji
wa majukumu yao na kubaini changamoto zao.
Bodi hiyo ikiongozwa na
Mwenyekiti Bwana Saulo Malauri, imefanya ziara hiyo leo tarehe 24 Oktoba, 2024
ikianzia katika Wilaya ya Kilolo katika Shirika la Kilolo Paralegal Unit na
kuelekea Iringa Mjini ambapo moja kati ya changamoto zilizoelezwa na watoa
huduma ni muingiliano unaoonekana ni wa kimaslahi na taasisi nyingine
zinazoshughulikia masuala ya haki.
Akimtaarifu Mwenyekiti wa Bodi na wajumbe wake, Bwana Manase ambaye ni Mratibu wa Shirika
hilo amesema kutokana na uhalisia kuwa mashirika ya msaada wa kisheria yanatoa
msaada wa kisheria bila malipo yeyote, mara kwa mara wamejikuta katika
mikwaruzano na baadhi ya taasisi na wananchi wengine ambao wanaendesha kazi za
huduma za kisheria kwa malipo kwa madai kuwa wanawapunguzia wateja.
Mwenyekiti wa bodi Bw. Malauri
akaelezea kuwa mchanganyiko huo unaoleta msuguano unatokana na uelewa mdogo juu
ya mipaka ya majukumu ambayo wasaidizi wa sheria wanatakiwa kuitambua na
kushauri elimu zaidi itolewe kwa umma juu ya ukomo kitu ambacho mtoa msaada wa
kisheria anakomea.
“Kinachojitokeza hapa na
kusababisha huu mwingiliano ni uelewa mdogo juu ya mipaka ya utekelezaji kwamba
paralegal anaanzia wapi mpaka wapi na hao wengine wanafanya nini! Naamini kuwa
hili likielimishwa basi hii migogoro itakwisha kwani paralegal hawaendi
Mahakamani” Alisema Mwenyekiti Malauri.
Aidha Mwenyekiti akatumia
nafasi hiyo kutoa rai kwa zile taasisi ambazo zinapenda kutumia migogoro ya
wananchi kama chanzo cha mapato kitu ambacho si kizuri kwa jamii lakini pia sio
tamanio la Serikali na pia sio sababu zilizopelekea kuanzishwa kwa sheria hizi.
Kwa upande wake Katibu wa Bodi
hiyo ambaye ni Msajili wa Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria na pia ni
Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria
Bi. Ester Msambazi alisema Kikao hicho cha siku mbili kilichojumuisha pia ziara
ya kuwatembelea watoa huduma ambapo bodi imeshuhudia hali halisi ya utekelezaji
kimekuwa na manufaa hasa katika kuelewa changamoto zinazohusiana na Msaada wa
Kisheria.
“Katika ziara hii tumeweza
kukutana na mambo mbalimbali ambayo yameisaidia Bodi kutambua changamoto hizo
kwa kuzishuhudia zikiwemo uhitaji wa wasaidizi zaidi wa kisheria kutokana na
jiografia ya maeneo husika lakini pia tumewasikia wasaidizi wakisheria wakiomba
‘refreshers course’ ili waweze kuendana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea
katika sheria na hilo ni suala ambalo tutalifanyia kazi,” alisema Msajili
Ester.
Aidha, Msajili alisema
anajipanga na timu yake kuhakikisha kuwa wanakuwa wanawatembelea wasaidizi wa
kisheria nchi nzima katika maeneo yao mara kwa mara kwa lengo la kuongeza
ufanisi na hivyo kupunguza mlundikano wa mashauri au migogoro ambayo yanaweza
kumalizikia katika ngazi hiyo ya chini na hivyo kumpunguzia gharama mwananchi
ambalo ndio lengo la uanzishwaji wa sheria hii.
Comments
Post a Comment