HAKI ZA BINADAMU ZIZINGATIE MAKUNDI YA WANAWAKE NA WANAUME - SAGINI
Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Jumanne Sagini akihutubia wakati akifungua kikao kazi cha kuandaa
taarifa ya Nchi ya utekelezaji wa Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu pamoja na Itifaki
ya Maputo ya Haki za Wanawake Afrika, Oktoba 23, 2024 Morogoro.
Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Jumanne Sagini kwenye picha ya pamoja na washiriki wa kikao kazi
cha kuandaa taarifa ya Nchi ya utekelezaji wa Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu pamoja na Itifaki
ya Maputo ya Haki za Wanawake Afrika, Oktoba 23, 2024 Morogoro.
xxxxxxxxxxxxxxxxx
Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Jumanne Sagini (Mb) ameitaka timu ya Wataalam kutoka Tanzania Bara
na Zanzibar inayoshiriki katika kuandaa na kukamilisha rasimu ya taarifa ya
Nchi kuhakikisha taarifa zinazoandaliwa katika kuimarisha Haki za Binadamu zinajumuisha
jinsia ya Kike na Kiume na kuepuka kuimarisha kundi moja pekee kwani
makundi haya yanategemeana.
Naibu Waziri Sagini ameyasema
hayo Oktoba 23, 2024 katika ukumbi wa Flomi hoteli mjini Morogoro wakati
akifungua kikao kazi cha kuandaa taarifa ya Nchi ya utekelezaji wa Mkataba wa
Afrika wa Haki za Binadamu na Watu
pamoja na Itifaki ya Maputo ya Haki za Wanawake Afrika ambayo Nchi ya
Tanzania imeridhia.Naibu Waziri Sagini amesema kuwa yapo baadhi ya maeneo
Wanaume wameacha kutimiza wajibu wao wa msingi na kuwa wategemezi kwa
Wanawake kutokana na kutojengwa vizuri katika kutambua majukumu yao ya msingi.
"Upo umuhimu kama Nchi
tunapokazia Haki za Binadamu, Haki za Mtoto wa Kike, Haki za Wanawake tusisahau
Haki za Binadamu, Haki za Mtoto wa Kiume na Haki za Mwanaume. Katika jamii wapo
baadhi ya Wanaume wanakwepa kutekeleza majukumu yao na wanawaachia
Wanawake pekee. Tunapoimarisha Haki za mtoto wa kike tuhakikishe tunaimarisha
na haki za mtoto wa kiume na twende nazo pamoja kwa maana makundi haya
mawili yanategemeana. Kama upendeleo ulifanyika kwa watoto wa kiume ilikua ni
zamani sio kwa huyu anayezaliwa sasa. Hawa wote ni watoto wetu isije kutokea
tunapendelea mtoto wa kike na kupelekea wanaume wanapokuwa watu wazima
kushindwa kutimiza majukumu yao kutokana na jamii inavyokuwa imejengwa
kuamini."Alisema Sagini.
Naibu Waziri Sagini amesema
kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan imefanya mabadiliko chanya na ambayo
yanahitaji kuripotiwa kwa kuwa mstari wa mbele kutimiza matakwa ya Mkataba wa
Afrika wa Haki za Binadamu na Watu kwa kuwa Serikali inayozingatia
Utawala Bora na Sheria katika kuwahudumia Watanzania, bila upendeleo, udini, ukabila,
jinsia na bila kujali vyama vyao vya Siasa na misimamo mingine.
Wakizungumza kwa wakati
tofauti tofauti Mkurugenzi Msaidizi wa Haki za Binadamu Bw. Richard
Kilanga na Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu
ya Taarifa za Haki za Binadamu Bi. Beatrice
Mpembo wamesema jukumu la Wizara ya
Katiba na Sheria ni kupitia Mikataba na kuelezea jitihada zilizofanywa na
Serikali katika kutekeleza Mikataba hiyo kwa kutoa Haki sawa kwa wote bila
ubaguzi.
Wizara ya Katiba na Sheria imewakutanisha wadau hao ili kuandaa rasimu ya taarifa na pia taarifa hiyo inasaidia katika kuelezea mipango na mikakati ya Nchi katika kutatua changamoto zilizopo katika jamii.
Imeelezwa kuwa taarifa
ikiandikwa vizuri itasaidia kupunguza maswali yanayoweza kuibuliwa wakati wa uwasilishwaji wake.
Comments
Post a Comment