KABUDI MGENI RASMI MHADHARA WA KUMBUKUMBU YA BENJAMINI MKAPA
Waziri wa Katiba na Sheria
Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akitoa salamu za ufunguzi katika Mhadhara
maalum wa Hayati Benjamini Mkapa, Rais wa Awamu ya Tatu ulioandaliwa na Chuo
Kikuu Cavendish cha Uganda, Oktoba 01, 2024 katika ukumbi wa hotel ya Johari
Rotana Jijini Dar es salaam.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na
Lusajo Mwakabuku - WyKS Dar
Waziri wa Katiba na Sheria
Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi ameshiriki kama Mgeni Rasmi katika Mhadhara
maalum wa Hayati Benjamini Mkapa, Rais wa Awamu ya Tatu ulioandaliwa na Chuo
Kikuu Cavendish cha Uganda leo tarehe 01/10/2024 katika ukumbi wa hotel ya
Johari Rotana Jijini Dar es salaam.
Akitoa salamu za ufunguzi
katika mhadhara huo, Waziri Kabudi alisema kwake hii ni fursa adhimu kuhutubia
mkutano huu unaosherehekea maisha ya kiongozi aliyekuwa na maadili na
mchapakazi na kwamba kumbukumbu ya Benjamin Mkapa ina nafasi ya pekee katika
mioyo ya wengi kwani inatuwezesha kutafakari juu ya uongozi na maono ya mtu
ambaye maono yake yalivuka mipaka ya Tanzania.
“Tunaposherehekea urithi wa
aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin William Mkapa, kiongozi ambaye
ushawishi wake unaendelea kutengeneza maisha yetu ya sasa na yajayo, ahadi yake
ya kuongoza kwa heshima, maono, na uwajibikaji kwa watu wake ni urithi ambao
sote tunajitahidi kuudumisha. Urithi wake unaendelea kuishi katika mioyo ya
wale aliowaongoza.” Alisema Kabudi.
Waziri Kabudi alieleza pia
kuwa maisha ya Benjamin Mkapa ni mfano mzuri wa uongozi, diplomasia na uwezo wa
maono. Alikuwa Rais wa tatu wa Tanzania na Chansela wa pili wa Chuo Kikuu cha
Cavendish Uganda. Katika majukumu yote mawili, alifanya kazi bila kuchoka ili
kuimarisha uhusiano ndani ya Afrika Mashariki na katika bara zima.
Aliendelea kusema kuwa
Marehemu Mkapa alielewa umuhimu mkubwa wa utulivu wa kikanda, si tu kwa ajili
ya ustawi wa mataifa binafsi bali kwa ajili ya kuendeleza elimu, ukuaji wa uchumi,
na sekta binafsi katika Afrika iliyounganishwa.
Mhadhara huu ulioandaliwa na
Chuo Kikuu cha Cavendish Uganda ni mhadhara watatu baada ya kufanyika mihadhara
miwili ya awali iliyofanyika Novemba 2022 na 2023 Kampala, Uganda.
Comments
Post a Comment