"MAJAJI NA WAENDESHA MASHTAKA WAJENGEWE UWEZO KUENDESHA MASHAURI DHIDI YA BIASHARA HARAMU YA BINADAMU" - MASWI
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba
na Sheria Bw. Eliakim Maswi (katikati) akizungumza katika kikao kilichowakutanisha
wataalam kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ujumbe
kutoka Nchini Marekani wanaohusika na mapambano na ufuatiliaji dhidi ya
biashara ya usafirishaji haramu wa Binadamu. Tarehe 30 Oktoba, 2024 ofisi za Wizara
Mtumba, Dodoma.
Ofisa kutoka Ofisi
inayoshughulika utokomezaji na ufuatiliaji wa biashara ya usafirishaji
haramu wa Binadamu kutoka nchini Marekani Bw. Adam Blakeman amesema kuwa
Nchi ya Tanzania ni miongoni mwa Nchi zilizopiga hatua kubwa katika
mapambano dhidi ya biashara hiyo ukilinganisha na Nchi
nyingine barani Afrika.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba
na Sheria Bw. Eliakim Maswi amesema Nchi ya Tanzania imefanya jitihada
mahususi katika kupambana na usafirishaji haramu wa Binadamu ikiwemo
marekebisho ya Sheria mbalimbali na adhabu kali kwa watuhumiwa wa biashara
hiyo, licha ya uhaba wa rasilimali fedha na uwezo mdogo wa Wataalam wa
kada mbalimbali wakiwemo Majaji na Waendesha Mashtaka wenye Elimu
ya Mapambano dhidi ya biashara hiyo.
Bw. Maswi amesema hayo katika
kikao cha kubadilishana uzoefu wa mbinu zinazoweza kutumika dhidi ya
Usafirishaji haramu wa Binadamu kilichowakutanisha wataalam kutoka Wizara ya
Katiba na Sheria, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ujumbe kutoka Nchini Marekani
wanaohusika na mapambano dhidi ya usafirishaji haramu wa Binadamu
kilichofanyika tarehe 30 Oktoba, 2024 katika ukumbi wa Wizara Mtumba jijini,
Dodoma.
Maswi ameeleza kuwa ili kuweza
kuendana na wakati na kudhibiti biashara hiyo, Majaji na Waendesha Mashtaka ni
miongoni mwa kada zinazotakiwa kujengewa uwezo ambapo takwimu zinaonesha kuwa
Waendesha Mashtaka wanne waliopo kwenye kikosi kazi cha mapambano hayo
ndiyo waliojengewa uwezo kuhusiana na Mapambano hayo.
"Biashara ya Usafirishaji
Haramu wa Binadamu ni biashara inayowahusisha watu wenye fedha, hivyo hata
mapambano yake yanahitaji uwezo wa kifedha. Kwa upande wa Wizara ya Katiba na
Sheria yapo maeneo ambayo Wataalam wake wanahitaji kujengewa uwezo wakiwemo
Majaji na Waendesha Mashtaka ili kuweza kuwa na uelewa mpana na kuendesha
mashauri yanayohusiana na biashara hiyo." Alisema Katibu Mkuu.
Kwa upande wake Ofisa kutoka
Ofisi inayoshughulika Utokomezaji na ufuatiliaji wa biashara ya
usafirishaji haramu wa Binadamu kutoka Nchini Marekani Bw. Adam Blakeman
amesema kuwa Nchi ya Tanzania ni miongoni mwa Nchi zilizopiga hatua
kubwa katika mapambano dhidi ya biashara hiyo ukilinganisha na Nchi
nyingine barani Afrika.
Comments
Post a Comment