SERIKALI INA DHAMIRA THABITI YA KUWALINDA WATOTO DHIDI YA UKATILI
Naibu Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria Dkt. Franklin Rwezimula na Wakili Bonifasi K. Mwabukusi – rais wa TLS pamoja na Mawakili wakiwasili katika viwanja vya Mnazi Mmoja baada ya matembezi ya amani dhidi ya vitendo vya ukatili na mauaji kwa watoto tarehe 18/10/2024 jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya
Katiba na Ufuatiliaji Haki kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Beatrice
Mpembo akipokea tuzo ya cheti cha
udhamini kwa niaba ya Wizara ya Katiba na Sheria kwenye matembezi ya amani
dhidi ya vitendo vya ukatili na mauaji kwa watoto tarehe 18/10/2024
jijini Dar es salaam.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Katiba na Sheria Dkt. Franklin Rwezimula akiambatana na Wakili Bonifasi K.
Mwabukusi – rais wa TLS wakitembelea banda la kutolea huduma za masada wa
kisheria la Wizara ya Katiba na Sheria tarehe 18/10/2024
jijini Dar es salaam.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Katiba na Sheria Dkt. Franklin Rwezimula akimsikiliza Mteja katika banda la
Wizara ya Katiba na Sheria, tarehe 18/10/2024
jijini Dar es salaam.
Wakili wa Serikali kutoka
Katiba na Sheria Bi. Agness Mkawe akishiriki katika matembezi ya amani ya
kupinga ukatili dhidi ya watoto tarehe 18/10/2024 jijini Dar es salaam.
xxxxxxxxxxxxxxxx
Na
Lusajo Mwakabuku – WyKS Dar es salaam
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba
na Sheria Dkt. Franklin Rwezimula ameongoza matembezi ya amani na kushuhudia
utolewaji wa Msaada wa Kisheria dhidi ya vitendo vya ukatili na mauaji kwa
watoto, hafla iliyoandaliwa na Tanganyika Law Society (TLS) akimwakilisha Katibu
Mkuu wa Katiba na Sheria Bwana Eliakim Maswi.
Katika hafla hiyo iliyofanyika
tarehe 18/10/2024 Naibu Katibu Mkuu amemesema Tanzania ni moja ya nchi zenye
Mfumo wa Kisheria thabiti inayowalinda Watoto dhidi ya vitendo vya ukatili.
Hata hivyo, kutokana na kukua kwa maendeleo ya kiteknolojia, vitendo vya
ukatili dhidi ya Watoto vimekuwa vikiibuka katika namna tofauti tofauti. Jambo
hili, limepelekea Serikali kwa kushirikiana na wadau, kuendelea kuchukua hatua
na mbinu mbalimbali katika kukabiliana navyo.
Akivitaja baadhi ya vifungu
vya sheria vinavyomlinda mtoto, Naibu Katibu Mkuu alisema Sheria ya Mtoto Sura
ya 13, inatoa mfumo mpana wa haki na ulinzi wa Watoto dhidi ya unyanyasaji na
unyonyaji. Akaongeza kuwa Sheria inawapa jukumu wazazi na jamii kwa ujumla
kusimamia na kulinda haki za Watoto ikiwemo haki ya kupata elimu, afya, malazi,
chakula, malazi na kuwalinda dhidi ya vitendo vya kijinai kwa mujibu wa Sheria
za nchi.
“Ulinzi wa mtoto umeanzia
kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, kwani imeweka mifumo ya kisheria
wa ulinzi wa haki za watoto. Kupitia, Ibara ya 14 inatambua haki ya kuishi,
wakati Ibara ya 13 inahakikisha usawa mbele ya Sheria na ulinzi dhidi ya
ubaguzi wa aina yoyote. Masharti haya ni muhimu kwani yanaweka msingi wa
kuwalinda watoto dhidi ya ukatili na ubaguzi,” alisema Dr. Rwezimula.
Akitoa salamu za awali kabla
ya kumkaribisha mgeni rasmi, Wakili Bonifasi K. Mwabukusi – rais wa TLS
aliwataka watanzania wote kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha kwenye daftari
la wapiga kura ili waweze kuchagua viongozi wanaodhani wanafaa na watakaoweza
kulinda haki za watoto.
Kutokujiandikisha kupiga kura
ni ukatili kwa Watoto, kutojiandikisha kunatoa fursa ya kupata viongozi wasio
bora ambao watashindwa kulinda haki za Watoto. Hivyo hata nyie Mawakili
msipojiandikisha maana yake mnakuwa mawakala wa ukatili huu. Jitokezeni
kujiandikisha na pia wote tupige kura”.
Alisema Mwabukusi.
Aidha Mwabukusi akatumia
nafasi hiyo kuipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuwa Wizara haijawajengea
ukuta bali imekuwa “Proactive” huku akihimiza Wizara taasisi nyingine ziige
mfano wa MoCLA na kutoiogopa TLS kwani Kazi ya TLS ni kuhakikisha utawala bora
na si vinginevyo.
Akisoma risala ya Mawakili wanawake wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Wakili Laetitia Petro Ntagazwa ambaye ni Makamu wa rais wa TLS na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi alisema wanashukuru kwa kiasi kikubwa kwani Serikali imeendelea kuonesha ushirikiano mzuri hasa mara baada ya uongozi mpya wa TLS kuingia madarakani na wakaomba Serikali iweze kuwatengea bajeti katika utekelezaji wa majukumu yao. Pia wakaishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana nao kupitia Mradi wa Mama Samia Legal Aid Kampeni na wakaahidi kuendelea kushirikiana vema kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.
Comments
Post a Comment