WAZAZI ANDIKENI WOSIA KUEPUSHA MIGOGORO YA MIRATHI – SAGINI
Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Jumanne Sagini (Mb) amesema kuwa chanzo kikuu cha matatizo ya
mirathi ni wazazi kutoandika wosia na kusabisha wajane na warithi halali
kudhulumiwa mali baada ya mzazi mmoja hasa baba kufariki.
Mhe. Sagini ameyasema hayo leo
Oktoba 21, 2024 wakati alipokuwa akifungua Mafunzo kuhusu Huduma za Wakala
wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa Makatibu Tawala, na Maofisa Ustawi wa
Jamii wa Halmashauri za Mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera, Geita, Simiyu na
Shinyanga kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kanisa Katoliki Kyabakari katika Wilaya
ya Butiama mkoani Mara.
"Naamini kila mmoja wetu
ameshakutana na shauri la aina hii katika eneo lake la kazi hivyo naamini elimu
tunayoipata leo itatusaidia kuweza kuwashauri na kuwasaidia wananchi namna ya
kupata haki zao hivyo tutumie fursa tunazozipata za kukutana na wananchi
kuwashauri waandike wosia. Kwa kufanya hivyo itasaidia kulinda haki za warithi
halali na pia tuwasisitize wananchi wafanye kazi na sio kusubiri ndugu afe ili
arithi mali hata kama yeye sio mmoja ya warithi wanaotambulika kisheria. Tuwaelimishe
wananchi kwamba Wosia sio uchuro kwani wapo wananchi wengi ambao wameandika
wosia muda mrefu uliopita na bado wanaishi," amesema Mhe. Sagini.
Pia Mhe. Sagini amesema kuwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa
akisisitiza kuwa Taasisi za Umma zitumie TEHAMA kuwawezesha wananchi kupata
huduma na mifumo ya TEHAMA baina ya Taasisi za Umma iweze kusomana ili
kupunguza usumbufu kwa wananchi, ambapo amewapongeza RITA kwa kubuni mfumo wa
eRITA ambao unawawezesha wananchi kutuma maombi ya kupata huduma kidijitali
bila kufika Ofisi za Wakala kwani mfumo huo umeongeza wigo wa upatikanaji wa
huduma hiyo kwa wananchi hata walio maeneo ya vijijini.
Aidha Kabidhi Wasii Mkuu na
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) Ndg.
Frank Kanyusi Frank, amesema kuwa mafunzo hayo yanayotolewa katika Mikoa ya
Kanda ya Ziwa yataweka mikakati madhubuti ndoa za kimila kusajiliwa na kuongeza
kuwa kwa sasa mipango ya Serikali inategemea watoto wote wawe wamesajiliwa
kufikia mwaka 2025.
Comments
Post a Comment