WAZIRI KABUDI AHIMIZA USHIRIKIANO KWA TAASISI ZINAZOSIMAMIA HAKI JINAI
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini
Bw. Sylvester Mwakitalu akizungumza katika kikao cha Utatu, 10 Oktoba, 2024 Jijini
Dodoma.
Baadhi ya Wakuu wa
Taasisi zinazounda Utatu pamoja na Wakuu wa Mashtaka Mikoa, Wakuu wa Upelelezi
Mikoa na Wakuu wa TAKUKURU Mikoa wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi wakati akifungua kikao cha Umoja huo
tarehe 9 na 10 Oktoba, 2024 Jijini Dodoma.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Waziri wa Katiba na Sheria
Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi amezitaka taasisi zinazosimamia masuala ya
Haki Jinai kuhakikisha kuwa wanasimamia na kuendeleza umoja na mshikamano
waliouanzisha unaojulikana kama Utatu, ili kuongeza weledi na ufanisi katika
kulinda Haki za watu wote kwa kufuata misingi ya Katiba na Sheria.
Waziri Kabudi amebainisha hayo
tarehe 9 Oktoba, 2024 jijini Dodoma, wakati akifungua kikao cha Menejimenti ya
taasisi zinazounda Utatu ikihusisha Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,
Ofisi ya Mkurugenzi wa upelelezi wa Makosa ya Jinai na Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa Nchini kikao ambacho pia kilihudhuriwa na Wakuu wa Taasisi
za Utatu kutoka Mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Prof. Kabudi amesema kuwa
Taasisi zinazosimamia Haki Jinai Nchini zinatakiwa kuendelea kutekeleza
mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha kuwa Wananchi wanapata
Haki zao kwa wakati ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa weledi, kuzingatia
misingi ya haki ili kuhakikisha amani, utulivu na umoja vinametamalaki kwa
maendeleo ya Nchi.
"Nikiangalia ushiriki wa
Viongozi katika ngazi zote ni ishara kwamba mnathamini dhamana ambayo mmepewa.
Kazi hii mnayoifanya kupeleleza, kuchunguza, kuendesha mashauri ya Jinai Nchini
pamoja na kuwa na ushirikiano huu kwa ajili ya kutathmini mafanikio na changamoto
zinazowakabili na namna ya kuzipatia ufumbuzi na kwa sasa tunapojiandaa
kuelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwakani niwaombe
mkasimamie Sheria zinazoongoza katika utendaji wenu ipasavyo ili
kuhakikisha umoja wa Nchi yetu, usalama wa Nchi yetu amani ya Nchi yetu
vinaendelea kuwepo." Alisema Kabudi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu amesema umoja huo wa Utatu uliundwa kwa
lengo la kurahisisha utendaji wao wa kazi na pia kutatua changamoto
wanazokumbana nazo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ambazo kwa namna moja
ama nyingine zinachelewesha ama kukwamisha haki za watu.
"Tuliamua kila mwaka tuwe
tunakutana Menejimenti ya Utatu na Viongozi wa ngazi za mikoa ili kujadiliana
na kutathmini yale ambayo tumeyafanya pamoja na kuweka mikakati ya mwaka
mwingine unaokuja, na tumekuwa na mijadala mizuri, mawasiliano na mada
mbalimbali na kuongeza ufanisi katika majukumu yetu". Amefafanua hayo
Mkurugenzi DPP.
Naye pia Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kamishna Ramadhani Kingai amesema ushirikiano wao
umeleta manufaa makubwa kwao katika utekelezaji wa utoaji haki katika
jukwaa la haki jinai.
"Ni rai yangu kuendeleza
na kuimarisha ushirikiano huu hususan katika kushughulikia makosa yanayovuka
mipaka hivyo ni muhimu kukuza ushirikiano huu sio tu kwa Taasisi zetu bali pia
taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi." Amebainisha hayo DCI Kingai.
Sambamba na hilo Mkurugenzi wa
Mashtaka Zanzibar Bw. Mgeni Jailan Jecha ametoa pongezi na shukrani kwa
Menejimenti ya Bara kwa mwaliko wa ushiriki katika kikao hicho cha Utatu kwani
kutasaidia kuzidi kuimairisha mashirikiano ya sekta za Jinai baina ya
Bara na Zanzibar, pia kujifunza na kupata uzoefu wa utendaji na kuchukua yale
ambayo yatatokana na kikao hicho cha Utatu.
Comments
Post a Comment