WAZIRI KABUDI APOKEA TAARIFA NANE ZA MAPITIO YA SHERIA
Mwenyekiti wa Tume ya
Kurekebisha Sheria Nchini (LRCT) Mhe. Jaji Winfrida Korosso akiongea
wakati wa hafla ya kukabidhi taarifa nane za tafiti za mapitio ya
Sheria zilizofanywa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 na Tume hiyo,
16 Oktoba, 2024. Mtumba jijini Dodoma.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Waziri wa Katiba na Sheria
Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi amepokea taarifa nane za tafiti za mapitio
ya Sheria zilizofanywa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 na Tume
ya Kurekebisha Sheria Nchini (LRCT), ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu
ya Tume katika kufanya tafiti na mapitio ya Sheria za Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa lengo la kuziboresha na kuzifanya ziendane na wakati uliopo.
Akiwasilisha taarifa ya tafiti
hizo wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika Oktoba 16, 2024
katika ukumbi wa Wizara Mtumba, jijini Dodoma Mwenyekiti wa Tume ya Kurebisha
Sheria Mhe. Jaji Winfrida Korosso amesema kuwa maandalizi ya taarifa hizo
yamehusisha hatua mbalimbali ikiwemo uchambuzi wa hoja za awali, tafiti,
mapitio ya uwandani, ukusanyaji na uchambuzi wa maoni ya wadau na maandalizi ya
taarifa husika.
Kwa upande wake Waziri
Kabudi ameipongeza Tume kwa kazi inayofanya katika kufanya maboresho ya
Sheria yenye tija na amesema kuwa taarifa hizo ni sehemu ya utekelezaji wa
mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai katika kusimamia mnyororo mzima
wa utoaji Haki Nchini ili kuimarisha Utawala Bora na kulinda Utu wa
Binadamu.
"Tunahitaji kufanya
mageuzi ya kimuundo na kuifanya Tume kuwa taasisi ya utafiti inayojitegemea
ambayo itakuwa chanzo cha fikra za Kisheria cha Serikali (think
tank) kama zilivyo taasisi nyingine za utafiti hapa Nchini."
Waziri Kabudi aliendelea
kusema "Sekta ya Sheria inapitia changamoto na adha mbalimbali
hususan za kiutendaji katika mchakato wa upatikanaji wa Haki kwa wakati ambapo
Wizara pamoja na taasisi zake inaweka mifumo rahisi itakayowezesha Taasisi za
usimamizi wa Sheria na utoaji Haki zinastahimili mahitaji ya jamii kwa mujibu
wa Sheria za Nchi na kuimarisha utawala Bora."
Waziri Kabudi ametoa rai na
amesema Wizara itaanda mapendekezo na kuona namna itakavyoweza kulifanya kuwa
takwa la Kisheria kwa taasisi zote Nchini zinazohitaji kufanya
Marekebisho ya Sheria kupeleka mapendekezo yao ya nia ya kufanya Marekebisho ya
Sheria kwenye Tume ya Kurekebisha Sheria ili ifanye utafiti na kutoa
mapendekezo ya maboresho ya Sheria ili kuhakikisha yanatija kwa Taifa.
Comments
Post a Comment