MSLAC KUTATUA MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI KILOSA
Waziri wa Katiba na Sheria
Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema Wilaya ya Kilosa imekuwa ikikabiliwa na
migogoro mingi ikiwemo ya wakulima na wafugaji na kwamba imekuwa makao makuu ya
migogoro ambayo mwarobaini wake ni Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia
- Mama Samia legal Aid Campaign.
Waziri Ndumbaro amebainisha
hayo Desemba 15, mwaka huu wakati akizindua kampeni ya msaada wa kisheria ya
Mama Samia katika kata ya Magomeni Wilayani Kilosa Mkoani humo ikiwa ni siku ya
pili baada ya kampeni hiyo kuzinduliwa Kimkoa Disemba 13, 2024.
Zaidi, Waziri huyo amesema
migogoro inayowakabili wananchi wa Kilosa kumeifanya Wizara ya Uvuvi na Mifugo
kuteua Kilosa kuwa makao makuu ya migogoro ya wakulima na wafugaji, hivyo
ameitaka timu ya wanasheria wa kampeni hiyo kuandaa ripoti itakayoonesha migogoro
iliyotatuliwa na ambayo haijatatuliwa ili ambayo haijatatuliwa ifanyiwe
oparesheni maalum ya siku kumi kuhakikisha inaisha.
"Na mimi niseme sasa
baada ya siku hizi kumi itaandaliwa ripoti yenye kuainisha migogoro ipi
imekwisha na ipi imesalia ile ambayo imesalia tutakuja na operesheni maalum
kumaliza migogoro hiyo." Amesema Mhe. Damas Ndumbaro.
Sambamba na hayo, amewataka
wananchi wa Mkoa wa Morogoro kujitokeza kwa wingi kwenye kampeni hiyo mara
itakapofika katika maeneo yao kwa lengo la kupata usaidizi wa kisheria ili
kusuruhisha migogoro yao kwa kufuata misingi ya sheria ili haki ipatikane bila
kumuonea mwingine.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa
wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amemuomba Waziri wa Katiba na Sheria
kuongezewa muda wa kampeni hiyo kwani amesema Wilaya hiyo ni kubwa ambapo Kata
10 na Vijiji 30 pekee vilivyobainishwa kufanyika kampeni hiyo haitakidhi haja
ya wananchi wengi wa Wilaya hiyo kufikiwa na Kampeni hiyo.
Wilaya hiyo inakabiliwa na
migogoro mingi hususan ya wakulima na Wafugaji, migogoro ya kijamii ikiwemo
ukatili wa jinsia ya wanawake na watoto, mirathi na ardhi, hivyo kufika kwa
msaada huo wa kisheria kutatatua kero nyingi za kijamii Wilayani humo na Mkoa
kwa ujumla.
Mbunge wa Jimbo la Kilosa
ambaye pia ni Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Mhe. Prof.
Palamagamba Kabudi amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kutumia ujio wa Kampeni ya
Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kupata ufumbuzi wa migogoro yao.
Comments
Post a Comment