RAIS SAMIA ANATAKA MIGOGORO IFIKIE MWISHO - WAZIRI NDUMBARO
Akizungumza wakati wa uzinduzi
wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika Wilaya ya Kilombero
Kijiji cha Mkamba, tarehe 14 Desemba, 2024 Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt.
Damas Ndumbaro amesema kuwa Kampeni hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwa ni kuonesha
mapenzi makubwa aliyonayo kwa Watanzania kwa kuwafikishia huduma za Msaada wa
Kisheria bure.
Waziri Ndumbaro amesema kuwa,
utekelezaji wa Kampeni hiyo utawasaidia Wananchi katika utatuzi wa Changamoto
za Kisheria ikiwa ni pamoja na kupeleka huduma za Msaada wa Kisheria karibu na
Wananchi.
"Utoaji wa Msaada wa
Kisheria bure kwa Watanzania ni jambo ambalo halijawahi kutokea tangu Uhuru.
Hii inaonesha ni kwa namna gani Rais anawajali Wananchi wake."Alisema
Ndumbaro.
Aliendelea kusema,
"Utekelezaji wa Huduma ya Msaada wa Kisheria ni maelekezo mahususi yaliyotolewa
kwa Wizara na Mhe. Rais ambapo aliiagiza Wizara iandae Programu itakayomwezesha
kila Mtanzania kupata Msaada wa Kisheria bure kwa Watanzania." Alisema.
Mkurugenzi wa Huduma za Msaada
wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Ester Msambazi amesema kuwa
Kampeni hiyo imekuwa na mwitikio mkubwa katika maeneo ambayo imeshatekelezwa na
imewawezesha Wananchi kupata elimu na misaada mbalimbali ya Kisheria.
Ametoa wito kwa Wananchi wenye
changamoto za Kisheria katika Mkoa wa Morogoro kujitokeza kwa wingi katika muda
huu wa Kampeni ili kuweza kuwasilisha migogoro yao.
Awali Mkuu wa Wilaya ya
Kilombero Mhe. Dunstan Kyobya amesema changamoto kubwa zinazoikabili Wilaya
hiyo ni pamoja na Wananchi kuvamia katika maeneo ya hifadhi, migogoro ya ardhi,
migogoro ya Wakulima na Wafugaji, mgawanyo wa mali na migogoro ya ndoa.
Kampeni hiyo inayotekelezwa
katika Halmashauri za Mkoa wa Morogoro ilizinduliwa rasmi tarehe 13, Desemba
2024 na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro na inatarajiwa kutekelezwa
kwa muda wa siku 9 ambapo Mkoa wa Morogoro ni Mkoa wa 11 tangu kuanza kwa
utekelezaji wa Kampeni hiyo.
Comments
Post a Comment