UONGOZI WA MAHAKAMA YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU NA WATU YAKUTANA NA VIONGOZI WA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA
Waziri wa Katiba na Sheria
Mhe. Prof Palamagamba John Kabudi tarehe 04 Desemba, 2024 amekutana na kufanya
kikao na Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu Mhe. Jaji
Imani Aboud aliyeambatana na ujumbe kutoka Mahakama hiyo iliyopo
jijini Arusha.
Katika mazungumzo hayo
yaliyofanyika katika ukumbi wa Wizara Mtumba, jijini Dodoma viongozi hao
wamejadili kuhusu nafasi ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na
Watu katika kusimamia na kulinda Haki za Binadamu na Watu wa Afrika.
Waziri Kabudi amesema yapo
maeneo ambayo yanahitaji kuboreshwa zaidi katika Mahakama ili kuimarisha
mahusiano mazuri yaliyopo ambapo pia wamejadili changamoto zinazoikabili sekta
ya Mahakama ambapo wamekubaliana kuendeleza majadiliano kwa ajili ya kuzifanyia
kazi changamoto hizo ili kuiwezesha Mahakama kutimiza majukumu yake ambayo
imepewa chini ya Mkataba wa kuanzishwa kwa Mahakama hiyo.
Sambamba na hilo maeneo mengi
ya majadiliano ni pamoja na kuimarisha ushirikiano katika eneo la Rasilimali
Watu ili kuwajengea uwezo Maafisa wa Mahakama kwa kupata mafunzo na uzoefu
katika Mahakama hiyo ili Tanzania iweze kutoa mchango wake katika utekelezaji
wa kazi za Mahakama hiyo.
Viongozi hao pia wamepitia
mambo ambayo Tanzania inawajibu wa kuyatekeleza chini ya Mkataba wa kuwa
Mwenyeji wa Mahakama hiyo.
Katika hatua nyingine Waziri Kabudi
amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kuridhia kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo kubwa la
Mahakama Afrika, ambapo amesema kuwa mambo mengi yanayofanywa katika Mahakama
hiyo yanaendana na utekelezaji wa falsafa ya 4R ya Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo ni Maridhiano,
Ustahimilivu, Kuboresha na Kujenga upya.
Waziri Kabudi amesema kuwa kwa
sasa Wizara inaandaa Muswada wa utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki
Jinai na katika kufanya hivyo miongoni mwa nyaraka zitakazotumika ni pamoja na
maamuzi ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.
Comments
Post a Comment