VIJANA WATOA MSAADA WA KISHERIA WAMPONGEZA KM MASWI
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba
na Sheria Bw. Eliakim Maswi akipokea zawadi kutoka kwa Vijana watoa Msaada wa
Kisheria waliojiunga na Wizara ya Katiba na Sheria miezi minne iliyopita kwa
ajili ya mafunzo kwa vitendo. Vijana hao wapatao 12 waliowakilishwa wameoneshwa
kuguswa na utendaji kazi wa Katibu Mkuu na moyo wa kuwajali. Tarehe 10 Januari, 2025
Mtumba, Dodoma.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Ikiwa ni miezi minne tangu vijana wapatao 12 wenye taaluma ya
Sheria walipojiunga na Wizara ya Katiba na Sheria na kushirikiana na Wataalamu
wa Wizara katika mafunzo kwa vitendo vijana hao wameonesha kuguswa na
kumkabidhi zawadi ya pongezi Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Eliakim Maswi kwa
utendaji kazi wake na moyo wa kuwajali.
Wakizungumza mara baada ya kumtembelea Katibu Mkuu ofisini kwake
Mtumba, jijini Dodoma leo tarehe 10 Januari, 2025 mwakilishi wa vijana
hao Prisila Kayuli amesema kuwa kwa kipindi chote wameshiriki na kupata
ushirikiano ipasavyo katika shughuli mbalimbali za Wizara bila kuwa na ubaguzi
jambo ambalo limewafanya wao kuwasilisha pongezi hizo ili kumtia moyo na kutambua
mchango wake kwa kulitambua kundi hilo la vijana katika kuhakikisha
wanapikwa ipasavyo katika sekta ya Sheria ili baadaye wawe Watendaji bora na
wenye maadili.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Bw. Eliakim Maswi amewataka vijana
hao kuendelea kujifunza kwa bidii pindi wanapopata nafasi kama hizo,
kumtanguliza Mungu na pia kuhakikisha wanakuwa na ndoto za kufika mbali.
Maswi ameongezea kuwa, furaha yake ni kuona Wataalamu wa
Wizara na wale wanaofika katika Wizara kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali
wanakuwa ni wachapakazi, wabunifu ili sekta ya Sheria iwe na Wanasheria
wenye weledi katika kazi na wanaoweza kusimama bila woga na bila
kubabaishwa katika kutetea maslahi ya
Taifa la Tanzania.
Comments
Post a Comment