WATOA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA 100 MKOANI MTWARA WAPIGWA MSASA
Waratibu 100 wa Kampeni ya
msaada wa kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid campaign) kutoka Halmashauri
tisa za mkoa wa Mtwara wamepatiwa mafunzo ya utekelezaji wa kampeni hiyo kuelekea kuanza kwa utoaji huduma ya kisheria
kwa wakazi wa mkoa huo ambayo yataanza Januari 24 hadi Februari 2, mwaka huu.
Akiongea wakati wa kuzindua
mafunzo hayo Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Bi. Bahati Geuzye amewataka
waratibu hao kuhakikisha kwamba mafunzo wanayopatiwa kuhusiana na kampeni hiyo
yanakuwa chachu na kuwawezesha kuwahudumia wananchi ambao kwa kiasi kikubwa
wamekuwa na uhitaji wa kupata huduma za msaada wa kisheria ili kuwasaidia
kutatua changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili.
Bi. Geuzye amesisitiza kuwa,
wananchi watakapokuwa na uelewa wa masuala hayo ya kisheria kutasaidia kuondoa
migogoro iliyopo baina yao na kufuata taratibu rasmi za kisheria katika masuala
mbalimbali.
"Kipekee kabisa
tunamshukuru Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuwezesha
kwa hali mali, na kuhakikisha tunakuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma za
msaada wa kisheria katika jamii, kama ambavyo jina la kampeni hii linasema
limebeba jina la Rais wetu mpendwa ikionesha nia yake thabiti ya kuhakikisha
kwamba wananchi wote wanapata haki" ameeleza.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu
Wizara ya Katiba na Sheria, ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Sheria kwa
Umma, Bw. Abdulrhaman Mshamu ameeleza kuwa lengo kuu la Kampeni ni kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa
wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria nchini.
Amefafanua kuwa, kampeni
imejikita katika kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi hususan katika masuala ya
ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, mirathi, usuluhishi wa migogoro kwa
njia mbadala, na masuala yahusuyo haki za binadamu kwa ujumla.
"Utekelezaji wa kampeni
hii ni utekelezaji wa sheria ya Msaada wa kisheria namba 21 ya mwaka 2017
iliyotoa wajibu kwa serikali kuhakikisha inafikisha huduma za kisheria kwa
wananchi wote" ameeleza.
Mikoa 11, imefikiwa na Kampeni
ya msaada wa kisheria ya Mama Samia tangu kuanza mwaka 2023 na mwaka huu 2025
inaendelea katika mikoa sita ikiwemo mkoa wa Mtwara.
Comments
Post a Comment