WATOA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA MSLAC LINDI WAPATIWA MAFUNZO
Mkurugenzi Idara ya Msaada wa
Kisheria Bi. Ester Msambazi akizungumza na Wananchi wa Ruangwa Mkoani Lindi
kupitia Redio Ruangwa ikiwa ni sehemu ya kutoa elimu ya Kampeni ya Msaada wa
Kisheria ya Mama Samia na kuhamasisha Wananchi wa Mkoa wa Lindi kujitokeza
katika uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria tarehe 19 Februari,
2025 Mkoani Lindi.
xxxxxxxxxxxxxxx
Wizara ya Katiba na Sheria imeendesha
kikao cha mafunzo kwa Wataalam watakaoshiriki katika utoaji wa huduma ya msaada
wa kisheria Mkoani Lindi kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia
(Mama Samia Legal Aid Campaign) yenye lengo la kutoa elimu mbalimbali za
Kisheria pamoja na utatuzi wa migogoro.
Akifungua kikao hicho kwa
niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Bwana. Nathalis Linuma ametoa rai kwa
washiriki wa kikao hicho kuzingatia na kutumia mafunzo hayo kama chachu na
mwangaza wa kuwasaidia wananchi kwa kuwapatia huduma za msaada wa kisheria
katika kipindi cha kampeni.
"Ni matarajio yangu kuwa
mtafuata mwongozo wa utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia
utakaotolewa na wataalam wa Wizara ili kuhakikisha kampeni inawanufaisha
walengwa hususan wananchi wasio na uwezo wa kumudu gharama za Mawakili, ni
vyema kuhakikisha kila mwananchi anaguswa na kampeni hii ili kwa pamoja tuweze
kupunguza na kuondoa migogoro hususan ya kisheria inayowakabili wananchi"
Aidha, Bw. Linuma amewataka
wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo ya mikutano ili waweze kupata fursa
ya kujifunza kuhusu masuala ya kisheria na kupata nafasi ya kuwasilisha
mashauri yao ya kisheria ili kupata ufumbuzi na utatuzi wa shauri husika kwa
usahihi.
Kwa upande wake Mkurugenzi na Msajiri wa Watoa Huduma za Kisheria Bi. Ester Msambazi ameeleza kuwa Kampeni hii inatekelezwa katika Mikoa 26 yaTanzania bara na 5 ya Tanzania Zanzibar ambapo kati ya hiyo Mikoa 17 tayari imeshafikiwa.
"Uwepo wa kampeni hii
umetokana na ombwe kubwa la kisheria lililopo miongoni mwa wanajamii hivyo
kampeni imekuja kuleta uelewa wa masuala ya kisheria na elimu ya sheria
miongoni mwa wananchi pamoja na kutoa huduma ya msaada wa kisheria inayohusu
usuluhishi na utatuzi wa migogoro ikiwemo ya ardhi, jinai na madai pamoja na
masuala ya mirathi na wosia"
Msaidizi wa Jeshi la Polisi na
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Lindi, Joyce Kitesho ameeleza kuwa
wanatarajia kampeni hii itakua ni chachu ya kupunguza migogoro mingi
inayotokana na ukatili wa kijinsia ambayo waathirika wake wakuu ni
wanawake na watoto.
Comments
Post a Comment